Chama Cha Wananchi CUF kimesema watanzania wanahitaji kuleta mabadiliko katika kujenga uchumi imara wa nchi yao.

Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Prof. Ibrahim Haruna Lipumba ameeleza hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya saba saba garden Morogoro mjini, ikiwa ni mwendelezo wa operesheni mchaka mchaka iliyoanzishwa na Chama hicho kwa mikoa mbali mbali ya Tanzania.

Amesema uchumi wa Tanzania unaweza kuimarika iwapo serikali itaweka mipango imara ya kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na kutumia rasilimali za nchi kwa maslahi ya wananchi.

“Tunataka kila Mtanzania aweze kunufaika moja kwa moja na rasilimali za nchi hii, mapato yatokanayo na maliasili yanaweza kuwa makubwa, kwa nini wananchi nao wasinufaike?” alihoji Prof. Lipumba.

Amesema tatizo kubwa linaloikabili Tanzania kwa sasa ni uongozi usiokuwa na dira ya uhakika ya mabadiliko, na kutaka Watanzania wafanye maamuzi ya kubadilisha safu ya uongozi na kuwapa madaraka viongozi wenye dira watakaoweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi.

Amesema iwapo CUF kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi mwaka 2015 kitahakikisha kuwa kinatekeleza mipango yake ya kukuza na kuimarisha uchumi ili kunyanyua kipato cha wananchi.

“Morogoro kwa mfano ardhi yake inakubali kuotesha kila aina ya mazao lakini wananchi wake bado ni maskini kutokana na kutokuwepo mipango imara ya kuimarisha na kuendeleza kilimo”, alifafanua Prof. Lipumba.

Akizungumzia kuhusu vitambulisho vya Taifa, Prof Lipumba amewahimiza wananchi kujisajili ili kupata vitambulisho hivyo wakati utakapofika.

Amesema licha ya utambulisho wa Watanzania, lakini vitambulisho hivyo pia ni muhimu katika mipango ya maendeleo.

Amesema vitambulisho hivyo ambavyo vinatumia teknolojia ya kisasa na alama za mwili, vinaweza kutumika hata katika mgao wa gawio litokanalo na mapato ya rasilimali iwapo serikali itaamua kufanya hivyo.

“Serikali inaweza kabisa kutumia vitambulisho vya Taifa kuweza kupeleka gawiyo kwa wananchi, ukizingatia kwa mfano simu za mkononi hivi sasa zinatumika kama benki, kinachohitajika ni mipango imara ya dira ya mabadiliko”, aliongeza Mwenyekiti huyo wa CUF.

Amefahamisha kuwa miaka 51 ya uhuru bado Tanzania haijakuwa na umeme wa uhakika, hali inayosababisha wawekezaji kushindwa kuwekeza viwanda vikubwa na kuzorotesha maendeleo ya kiuchumi.

Nae Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad alisema rasilimali za nchi bado hazijawanufaisha ipasavyo Watanzania, na badala yake zimekuwa zikiwanufaisha zaidi wageni, jambo ambalo linahitaji kuangaliwa upya.

Amesema baadhi ya vyama vikuu vya siasa nchini tayari vimeonesha kupoteza mwelekeo, na kuwaomba wananchi kuendelea kukiunga mkono CUF ili kiweze kuleta mabadiliko ya kweli.

“Chama chetu siku zote kinaendelea kuhubiri juu ya dhamira yake ya kuwaunganisha Watanzania na kuleta mabadiliko ya kweli ya kiuchumi ili kila kila mwananchi apata haki sawa na mwengine, sambamba na kuondosha kabisa matabaka haya ya wananchi wa daraja la kwanza, la pili na la tatu”, alifafanua Maalim Seif.

Aliwapongeza wananchi wa Morogoro kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo licha ya kuibuka kwa mvua kubwa iliyosababisha mtafaruku na kuleta hofu ya kuvurugika kwa mkuano huo.

Alisema mvua hiyo ambayo imekosekana kwa kipindi kirefu mkoani humo, ni dalili tosha kuwa chama hicho ni chama cha Baraka, na kuwaomba wananchi wananchi wandelee kukiunga mkono ili kutimiza malengo yake.

Katika hatua nyengine aliyekuwa mwenyekiti wa vijana CHADEMA jimbo la Ukonga Mchungaji Calistus Titus aliweka wazi baadhi ya sababu zilimpelekea kujiengua katika chama hicho mwezi uliopita na kuamua kujiunga na CUF.

Mchungaji huyo wa kanisa la Gongo la mboto “Ulongoli B”, alisema alichoshwa na tabia ya viongozi wa chama hicho kutokana na jazba walizonazo katika kuendesha chama, pamoja na kuwepo ufisadi wa kutisha ndani ya chama hicho.

Alisema alivutiwa na CUF baada ya kuona kuwa viongozi wake ni watu wenye busara na mwelekeo thabiti wa kuleta ukombozi wa kweli kwa Watanzania wote.


Hassan Hamad, OMKR

0 comments:

 
Top