Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad leo amewaongoza maelfu ya waislamu katika sala ya mhadhiri mashuhuri wa Zanzibar Sheikh Nassor Abdalla Bachoo.


Sheikh Nassor Bachoo alifariki jana Chukwani Zanzibar, baada ya kuugua kwa muda mrefu, na kusaliwa katika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar.


Baada ya sala hiyo iliyohudhuriwa pia na viongozi mbali mbali wa kidini kutoka nchi jirani , msafara ulielekea katika kijiji cha Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa ajili ya mazishi.


Viongozi wengine mashuhuri waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, Kadhi Mkuu Sheikh Khamis Haji na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Mohd Aboud Mohd.


Sheikh Nassor Bachoo alianza kuugua kwa takriban mwaka mmoja uliopita ambapo mwishoni mwa mwaka 2012 alipelekwa nchini India kwa ajili ya matibabu zaidi.


Wakati akiugua na kupatiwa matibabu, Sheikh Nassor Bachoo aliwahi kuzushiwa kifo zaidi ya mara tatu, na kusababisha mwanawe kuanza kutoa taarifa katika vyombo vya habari kupotosha taarifa hizo, lakini hatma yake ilifikia jana.


Umati mkubwa ulijitokeza kumsalia katika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar wakiongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, na hatimaye kuzikwa katika kijiji cha Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Hassan Hamad, OMKR

0 comments:

 
Top