Baada ya ukimya mrefu na Jamii kulemaa katika kuangalia mchezo wa kandanda ndani ya Viunga vya uwanja wa Amani Mjini Zanzibar sasa mambo yamegeuka na wapenzi wa michezo wameshuhudia Mashindano ya Kimataifa ya Riadha { Zanzibar Island Run }.
Mashindano hayo yaliyoshirikisha wanariadha wa Kimataifa kutoka Kenya, Tanzania Bara na wenyeji Zanzibar yameandaliwa na Chama cha Riadha Zanzibar chini ya usimamizi wa Baraza la Michezo Zanzibar BMZ.

Wapenzi hao wa Michezo wameshuhudia ushindani mkali uliojichomoza na kupelekea burdani hiyo kuwa na raha za aina yake kwa vile imeshirikisha pia wanaridha wenye umri mrefu wakiwemo pia watu wenye ulemavu.

Matokeo ya mashindano hayo katika mbio za Kilomita 21.1 mshindi wa kwanza alikuwa Dicson Malwa kutoka Tanzania Bara, Mshindi wa Pili alikuwa Said Juma kutoka Zanzibar na Mshindi wa Tatu alikuwa Joseph Fransis kutoka Tanzania Bara.

Kilomita 21.1 wanawake mshindi wa kwanza alikuwa Sara Ramadhani kutoka KMKM Zanzibar, na wa pili alikuwa Fairuna Mohd kutoka Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA }.

Mbio za Kilomita Tano mshindi alikuwa Saba Daud Abdulla kutoka Zanzibar, wa pili ni Ahmad Gota wa JWTZ na kwa upande wa watu wenye ulemavu washindi walikuwa Othman na Haji.

Akizungumza mara baada ya kutoa zawadi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alishauri michezo kurejeshwa tana maskuli kwa lengo la kuirejesha Zanzibar katika medani bora ya Kimataifa.

Balozi Seif amelitaka Baraza la Michezo Zanzibar kuhakikisha linavisimamia vyema vyama vya Michezo Nchini katika kutekeleza kazi zake kwa umakini na uadilifu ili kuijengea mazingira bora Zanzibar katika kushindana badala ya kushiriki kwenye mashindano ya Kimataifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizungumza na wana michezo katika mashindano ya Kimataifa ya Michezo wa riadha yaliyofanyika kwenye uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.

Balozi Seif ameelezea kutia moyo kwake na ari mpya iliyoletwa na Wizara inayosimamia michezo Zanzibar kwa kushawishi vyama vya michezo kurejesha tena baadhi ya michezo ambayo imefifia na mengine kluifa kabisa.

Balozi Seif alisema maandalizi hafifu na migogoro mingi inayoendelea kuvukuta ndani ya Vilabu pamoja na vyama vingi vya michezo Nchini imeipunguzia sifa na heshima Zanzibar katika medani ya michezo katika mashindano ya Kimataifa.

“ Kwa muda mrefu tulichokuwa tukikisikia sana ni viongozi vya vyama vya michezo kugombana wenyewe kwa wenyewe. Ukiuliza chanzo cha migogoro hiyo unakuta ni matumizi mabaya ya fedha au kuwania uongozi”. Alikemea Balozi Seif.

Aieleza kwamba michezo mingi iliyokuwa ikitajikana Zanzibar hivi sasa imepungua au kufa kabisa pengine kutokana na vijana wengi kuelekeza nguvu zao katika mchezo wa soka ambao nao pia umepungua ari na mori iliyokuwepo awali.

Amesema vijana wengi nchini wameanzisha utamaduni mpya wa kupenda kushabikia mashindano ya nje ya nchi kitendo ambacho kimechangia kupunguza msisimko wa mashindano ya michezo ya ndani ya nchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba umefika wakati kwa Bazara la Michezo Zanzibar kupambana na hali hiyo na kuvitaka vyama vya michezo kuwa makini katika kujipangia ratiba za mashindano.

Balozi Seif alitahadharisha kwamba ni udhaifu mkubwa kwa chama kinachosimamia michezo ndani ya kipindi cha mwaka mzima kinakosa kuendesha mashindano ya aina yoyote.

“ Chama cha michezo kinapokuwa hakina ratiba ya mashindano maana yake chama hicho kimekufa kwani hakina kazi nyengine yoyote ya kufanya. Mimi binafsi nimefurahi nilipoalikwa kuja katika mashindano haya, nimeanza kuona kwamba baadhi ya vyama vya michezo vinaanza kuzinduka kuelewa wajibu wao”. Alielezea faraja yake Balozi Seif.

Aliwaeleza wana michezo hao kwamba msimamo wa Serikali Kuu hivi sasa ni kuziona timu zake zinashinda kila zinaposhiriki katika mashindano ya kimataifa na kuirejeshea heshima yake Zanzibar katika medani ya michezo.

Balozi Seif alishauri michezo ichangie sekta ya Utalii kwa kiwango kikubwa kwa vile mashindano kama riadha, marathoni, Triathlon na Maountain Bike yana sehemu kubwa ya kuvutia watalii kuingia nchini iwapo yataandaliwa vyema.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza mpango wa pamoja wa miaka mitatu ulioshirikisha wataalamu wa Kamisheni ya Utamaduni na wale wa Wizaea ya Elimu na Mafunzo ya Amali wa kuendeleza michezo maskulini.

Balozi Seif alisema hiyo ni hatua nzuri ya kuanzia na alielezea matumaini yake kwamba mpango huo utakapokamilika na kuanza kutumika utasaidia kuibua ari pamoja na vipaji vya wanafunzi hao.

Othman Khamis Ame 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top