Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ametaka tahadhari zaidi zichukuliwe katika kuwakuza watoto kimaadili, ili kuwaepusha na vitendo viovu na kujenga jamii iliyo bora.

Amesema iwapo watoto watakuzwa katika maadili mema wataweza kuepukana na vishawishi vya kujiingiza katika vitendo viovu vikiwemo utumiaji wa dawa za kulevya.

Maalim Seif ameeleza hayo alipokuwa akifungua tamasha la nne la Kiislamu Zanzibar, linalokwenda sambamba na kumbukumbu ya Sheikh Abdallah Saleh Farsy aliyefariki Novemba 1982, pamoja na wanazuoni wengine wa Zanzibar, katika hafla iliyofanyika Jumba la wananchi Forodhani.

Amefahamisha kuwa vitendo viovu katika jamii vimekuwa vikichangiwa kwa kiasi kikubwa na kuwepo kwa dhana ya utandawazi dunia, na kuwataka wazazi na walezi kushirikiana katika malezi ili kuwalinda watoto na vitendo hivyo.

Aidha Makamu wa Kwanza wa Rais ameelezea haja ya kuendelezwa kwa umoja wa waislamu katika nchi za Afrika Mashariki ambazo zina historia nzuri na ya muda mrefu katika kuendeleza ustaarabu na utamaduni wa Kiislamu.

Katika kufanikisha matarajio hayo Maalim Seif amesisitiza umuhimu wa kuwajengea watoto mazingira bora ya kielimu ili waweze kupata taaluma zote za dini na dunia ambazo zitaweza kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku.

Akizungumzia kuhusu tamasha hilo linalowashirikisha wanazuoni mbali mbali wa Afrika Mashariki amesema ni muhimu katika kuwaunganisha waislamu, kuendeleza ustaarabu pamoja na utamaduni wa kiislamu katika nchi za Afrika Mashariki.

Kadhi Mkuu Mstaafu wa Kenya ambaye alihudhuria ufunguzi huo Sheikh Hamad Muhammad Kassim Al-Mazrui ametoa wito kwa viongozi kuweka misingi bora ya uongozi, ili waweze kukumbukwa kutokana na michango yao waliyoitoa kwa jamii.

Ametoa mfano kwa Sheikh Abdallah Saleh Farsy ambaye amekuwa akikumbukwa kutokana na mchango wake wa kukuza maadili na kuendeleza dini ya Kiislamu katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.

“Kwanza nimefarijika sana kwa kupata fursa ya kushiriki katika tamasha hili muhimu kwa waislamu wa Afrika Mashariki, lakini pia nawaomba viongozi wetu waongoze vyema ili waache athari njema wakati wanapoondoka katika uongozi.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk amesema Zanzibar ni kitovu cha ustaarabu na elimu ya dini ya Kiislamu, na kutaka mambo hayo yaenziwe kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Ameahidi kushirikiana na jumuiya iliyoandaa tamasha hilo ya “Zenj Islamic Festival” katika kuhakikisha kuwa inafanya kazi zake vizuri, na kwamba inaisaidia serikali katika kuendeleza utamaduni wa Mzanzibari.

Mapema Mkurugenzi Mwendeshaji wa Jumuiya hiyo Sheikh Jabir Haidar Al-Farsy amesema jumuiya hiyo iliyoasisiwa miaka minne iliyopita, imekuwa ikipata faraja kutokana na kuungwa mkono na wadau mbali mbali wakiwemo watendaji wa serikali na taasisi binafsi.

Hafla hiyo ya ufunguzi wa Tamasha la nne la Kiislamu Zanzibar, ilihudhuriwa pia na wanazuoni mbali mbali wakiwemo Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali na mwandishi wa siku nyingi wa vitabu vya dini ya Kiislamu Sheikh Ali Abdalla Al-Maawiy, ambaye pia ni Rais na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waislamu Afrika Mashariki.

Hassan Hamad (OMKR  
    

0 comments:

 
Top