Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikuwa miongoni mwa Viongozi wa Serikali,Mashirika na Taasisi mbali mbali za Kimataifa walioshiriki kuweka saini kitabu cha maombolezi kufutia kifo cha Waziri Mkuu wa Zamani wa India Dr. Inder Kumar Gujral.

Dr. Inder Gujral alifariki dunia Ijumaa iliyopita katika Hospitali moja ya kiraia Nchini india ambako alikuwa amelazwa tokea tarehe 19 Novemba mwaka huu baada ya mafigo yake kushindwa kufanya kazi.

Akipokewa na Kaimu balozi mdogo wa India aliyepo hapa Zanzibar Bwana D.J Rao Balozi Seif alitia saini hiyo katika Ofisi ya Ubalozi huo iliyopo Migombani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Dr. Gujrat aliyefikia umri wa miaka 92 alishika madaraka ya kuwa Waziri Mkuu wa 12 wa India kuanzia tarehe 21 Aprili mwaka 1997.

Katika uhai wake akiwa mtumishi wa serikali aliwahi kushika nafasi za uwaziri katika wizara tofauti, Balozi wa India Nchini Urusi pamoja na mwenyekiti wa kamati ya Bunge la Nchi hiyo.

Katika Nyanja za Kimataifa Dr. Gujrat aliwahi kuwa mwenyekiti wa baraza la ushirikiano la Kusini mwa Asia, Mjumbe katika shirika la Unesco pamoja na mwakilishi wa umoja wa Mataifa katika kutatua baadhi ya mizozo Barani Afrika.

Kwenye harakati za Kisiasa na Uhuru Dr. Gujrat akiwa na umri wa miaka 11 alishiriki katika harakati za kudai uhuru wa Taifa hilo kwenye miaka 1931 hali iliyosababisha yeye na wenzake kuwekwa ndani na baadaye kufungwa jela mwaka 1942.

Katika uhai wake waziri Mkuu huyo wa zamani wa India Dr. Gujrat alikuwa akipenda kuandika vitabu mbali mbali pamoja na utangazaji kwenye hadhara za Kitaifa na Kimataifa.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amekabidhi mchango wa shilingi milioni moja kutekeleza ahadi aliyoitoa kwa uongozi wa Jumuiya ya Watu Wasioona Zanzibar { ZANAB } mwezi uliopita.

Mchango huo ameukabidhi kwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Bwana Mohd Kassim hapo Ofisini kwake vuga Mjini Zanzibar ukilenga kusaidia maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Zanab unaoanza tarehe 6 hadi 8 mwezi huu.

Balozi Seif ameutakia kila la kheir Mkutano huo na kutaraia Maazimio mazuri yatakayosaidia kuiwezesha Jumuiya hiyo kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ulio makini.

Aliuhakikishia Uongozi wa Jumuiya hiyo kwamba changa moto walizozieleza wakati wa Kikao cha tayari ameanza kuzichukulia hatua zinazostahiki likiwemo la bara bara inayoingia kwenye Ofisi yao iliyopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.

“ Nimepokea ripoti nzuri na yenye ufasaha inayoelezea matatizo yenu ambayo nilimtuma Mtendaji wangu kuyafuatilia na tayari kazi hiyo nimeshamuagiza Afisa wangu kwa hatua za utekelezaji”. Alifafanua Balozi Seif.

Wakati huo huo Balozi Seif alikabidhi Mchango wa Shilingi Milioni moja { 1,000,000/- } kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kijiji cha Bweleo Bwana Mataka Makame kwa ajili ya upigaji plasta wa Jengo jipya la Skuli ya Maandalizi ya Kijiji hicho.

Mchango huo umekuja kufuatia ziara yake aliyoifanya katika vijiji vya Bweleo na Bwefum kukaguwa shughulio za Maendeleo ya Wananachi wa Vijiji hivyo pamoja na kufahamu change moto zinazowakabili.

Balozi Seif aliwataka wananchi wa Kijiji hicho hasa waumini wa Dini ya kiislamu kuendelea kuwa wastahamilivu kutokana na ukosefu wa sehemu muwafaka ya kutawadhia na hatua anachukua ili kuona tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi.

Akitoa shukrani zake mara baada ya kupokea mchango huo Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kijiji cha Bweleo Bwana Mataka Makame alimueleza Balozi Seif kwamba juhudi za upatikanaji wa huduma ya maji katika Kijiji hicho ziko katika hatua ya kuridhisha.

Bwana Mataka alisema Wananchi wa Kijiji hicho wana matumaini ya kupata huduma hiyo ya majikatika kipindi kifupi kijacho baada ya kuikosa kwa a kwa muda mrefu kwa vile ufungaji wa Mashine pamoja na Mabomba unafikia ukingoni.

Othman Khamis Ame 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top