Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema kuendelea kuwepo kwa amani Nchini ni jambo la msingi linalowawezesha wananchi kupata faraja kwa kuendelea na shughuli zao za maisha za kila siku.
 

Alieleza hayo wakati akizungumza na Kamanda wa Brigedia Nyuki Zanzibar Brigedia General Sharif Sheikh Othman ambae alifika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Rais Jakaya Mrisho Kikwete kushika wadhifa huo hivi karibuni.
 

Balozi Seif alisema amani ya Nchi hupatikama na kuwa salama iwapo wale wanaolindwa ambao ni wananachi na wanaolinda wakiwa walinzi watakuwa na utamaduni wa kushirikiana pamoja.
 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Kamanda Mpya wa Brigedia nyuki kwamba Zanzibar bado iko salama licha ya cheche za vujo zilizowahi kujichomoza hivi karibuni ambazo zilifanywa na baadhi ya vijana kwa ushawishi wa kisingizio cha Dini.
 

Aliahidi kwamba Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambayo ndio inayoratibu masuala la Muungano na Taasisi zake itaendelea kushirikiana na Taasisi hizo likiwemo Jeshi la Wananachi katika kuona majukumu waliyopangiwa na Taifa wanayatekeleza kwa ufanisi uliokusudiwa.
 

 Hata hivyo Balozi Seif alisema Jeshi la Wananchi wa Tanzania pamoja na Baadhi ya Vikosi vyengine vya ulinzi vinaendelea kukabiliwa na migogoro ya ardhi kati ya nkambi zao na wananchi walipo karibu na maeneo hayo.


Balozi Seif aliendelea kusisitiza kwamba njia pekee ya kukabiliana na changa moto hizo ni kwa pande zinazohusika na migogoro hiyo kufikia mazungumzo kwa kuzipatia ufumbuzi changa moto zinazojichomoza.


“ Sisi kama Serikali tumekuwa tukiripotiwa migogoro mingi ya ardhi kati ya Wananchi na baadhi ya kambi za ulinzi mfano kama maeneo ya Kisaka saka, Unguja Ukuu, Dunga na hanyegwa mchana”. Alifafanua Balozi Seif.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Brigedia General Sharif Sheikh Othman kwa kufanya kazi kwa nidhamu wakati akiwa Mwambata katika Ubalozi wa Tanzania Nchini Misri.
 
Balozi Seif alisema juhudi hizo ndizo zilizomjengea heshima na kufikia hatua ya kupandishwa cheo na hatimae kuteuliwa kushika wadhifa huo mzito ambao anaamini kwamba atautekeleza kwa ufanisi mkubwa.
 
Mapema Akijitambulisha rasmi kwa Makamu wa Pili war Rais wa Zanzibar Balozi Seif Kambanda wa Brigedia Nyuki Zanzibar Brigedia General Sharif Sheikh Othman alishukuru mashirikiano mazuri anayoendelea kuyapata ndani ya kipindi kifupi tokea ashike wadhifa huo.
 
Kamanda Sharif alifahamisha kwamba msaada wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambao atauhitaji kila mara ni muhimu kwake katika kutekeleza majukumu aliyopangiwa na Taifa.


Othman Khamis Ame 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top