Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imezuia utolewaji wa Hati za umiliki wa maeneo ya Ardhi kwa ajili ya Kilimo kwa wakulima wa Vijiji vya Dole, Nguruweni na Ndunduke Dole kufuatia kujichomoza kwa hitilafu za umiliki wa maeneo hayo kwa baadhi ya watu na kusababisha migogoro kwa kipindi kirefu.

Uzuiaji huo umekuja baada ya malalamiko makali yaliyotolewa na Wakulima hao dhidi ya Watendaji na Maafisa wanaosimamia Ardhi, Kilimo wakiwemo pia Viongozi wa Ngazi za kati wa Serikali waliyokuwa wakiyawasilisha kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Malalamiko hayo ya Wakulima yaliyojaa shutuma na lawama waliyatoa hapo katika eneo la Skuli ya Jumuiya ya Wazazi iliyopo Dole Wilaya ya Magharibi yakishuhudiwa pia na Mwakilishi wa Jimbo la Dole na Mbunge wa Jimbo la Mfenesini.

Baadhi ya wawakilishi wa Wakulima hao wa Dole, Nguruweni na Ndunduke walimlalamikia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba tatizo hilo sugu lilikuwa likichangiwa na baadhi ya maofisa waliopewa jukumuj la kusimamia maandalizi ya utolewaji wa nyaraka kwa wakulima 28 wa awamu ya kwanza waliokubalika kupatiwa hati ya umiliki huo.

Walisema Maafisa hao walidiriki kutumia hadaa ya kuchokea majina ya Watu wengine ambao cha kusikitisha zaidi hawaishi wala kutambuliwa katika maeneo hayo ya wakulima.

“ Watendaji hawa wanaonekana kubeba kiburi na kujaa dharau hasa kutokana na kupinga utaratibu ulioridhiwa na Waziri Kiongozi wa awamu ya Sita wa kupatiwa hata kama eneo dogo la robo eka pale mkulima anapoendesha shughuli zake za Kilimo. Lakini chengine cha ajabu hata agizo la Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi wamelidharau”. Walisema Wakulima hao wakati wakitoa duku duku lao na huku wakiwaonyeshea vidole baadhi ya viongozi na watendaji waliochelewesha utaratibu huo.

“ Sisi hata kama tutamilikishwa vijisehemu vidogo vidogo tunavyoendeshea maisha yetu kwa kilimo basi tutakuwa radhi na kufurahia utaratibu huo utaotupa faraja ya maisha”. Walisema wakulima hao.

Walalamikaji hao wa Dole, Ndunduke na Ngurueni walimuomba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Serikali isisite kuwachukulia hatua kali na za kisheria watendaji wake wanaoshindwa kutekeleza maagizo ya Viongozi wa juu wa Serikali.

Walisema tabia hii ya kigugumizi iliyojengeka ndani ya vufua vya baadhi ya watendaji hao ndio inayochangia kuwapa kiburi kinachosababisha kujiamulia mambo kinyume na utaratibu kwa kuendeleza ubinafsi zaidi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali asili Zanzibar Nd. Afan Othman alisema Wizara hiyo itahakikisha inafanya utaratibu wa uhakiki wa maeneo hayo ambayo yalikuwa katika umiliki wa Wizara hiyo kabla ya kumilikishwa kwa Wakulima wa maeneo hayo.

Nd. Afan alisema uhakiki huo ambao baadhi ya wakulima hao walikuwa wakiuona kero utaiwezesha Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na ile ya Ardhi kuwepuka hitilafu ya kutokea eneo moja kumilikishwa zaidi ya watu wawili jambao ambalo linaweza kuzaa mgogoro mwengine mpya usio wa lazima.

Naye Mkurugenzi wa Ardhi Ndugu January Fusi alisema wakati umefika hivi sasa kwa kuiangalia upya sheria ya umiliki wa ardhi kwa ule utaratibu wa eka tatu tatu waliopewa wananchi kwa ajili ya kilimo mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Nd. January Fusi alisema ongezeko kubwa la idadi ya watu liliopo nchini hivi sasa limesababisha vurumai kubwa katika umiliki wa ardhi isiyoongezeka ambayo imekuwa mali zaidi miongoni mwa Wananchi na hata wawekezaji.

Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema amefikia maamuzi ya kuteua Kamati Maalum ya Viongozi Wanne watakayosimamia suala hilo na kulipatia ufumbuzi ndani ya kipindi cha miezi miwili kuanzia sasa.

Akishangiriwa kwa vifijo na makofi na wakulima hao Balozi Seif aliitaja Kamati hiyo mbele ya wakulima hao kuwa ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi.

“ Moja kati ya jukumu kubwa la Kamati hii ni kuhakiki maeneo yote na tufikie hatma ya kuyagawa maeneo haya kwenu nyinyi wakulima na nisingependa ikapindukia mwishoni mwa mwezi wa pili mwakani ”. Alifafanua Balozi Seif.

Aliwaeleza Wakulima hao kwamba ni faraja kwa serikali kuona wananchi walio wengi hivi sasa wameamuwa kulipa umuhimu unaostahidi suala la Kilimo ambacho ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaonya Viongozi na watendaji wenye tabia ya kunyanyasa Wananchi na hasa wakulima kuacha mara moja mtindo huo ambao unakwenda kinyume na dhamira na muelekeo wa Serikali.

“ Watu wanaopewa hati ya umiliki wa maeneo ya ardhi na baadaye kuanza kunyanyasa wananchi na wakulima waliomo ndani ya maeneo hayo kwa kuwaamuru waondoke hawafai katika Jamii na inafaa kutengwa kabisa”. Alisisitiza Balozi Seif.

Mgogoro wa maeneo ya ardhi kwa ajili ya Kilimo katika Viji vya Dole, Ngurueni pamoja na Ndunduke Dole umeibuka tokea mwanzoni mwa miaka 2000 na kuanza kushughulikiwa na Waziri Kiongozi Mstaafu Mh. Shamsi Vuai Nahodha.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top