Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alibadilishana Mawazo na Ujumbe wa Viongozi wanane wa Makampuni Tofauti kutoka Uholanzi ukiongozwa na Rais wa zamani wa Maseneta wa Bunge la Ulaya Bwana Rene Van Der Linden hapo nyumbani jkwake Namanga Jijini Dar es salaam

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuunda chombo Maalum kitakachoratibu na kusimamia masuala ya Mafuta na Gesi katika harakati zake za kujiimarisha Kiuchumi pamoja na kustawisha maisha ya Wananchi wake.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Ujumbe wa Viongozi wanane wa Makampuni tofauti ya uwekezaji Vitega Uchumi kutoka Nchini Uholanzi aliokutana nao hapo Nyumbani kwake Mtaa wa Haile Selassie Mjini Dar es salaam.

Balozi Seif alisema Zanzibar tayari imeshaiandikia Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuiomba suala la Mafuta na Gesi litolewe katika Mambo ya Muungano kwa lengo la kupata nguvu na fursa zaidi za Kiuchumi.

Aliueleza Ujumbe huo ulioongozwa na Rais wa zamani wa Maseneta wa Bunge la Ulaya Bwana Rene Van Der Linden ukiambatana pia na Balozi wa Uholanzi Nchini Tanzania Dr. Ad Koek koek kwamba chombo hicho kinatarajiwa kuwa na Mamlaka kamili ya Utafutaji, udhibiti na uendeshaji wa Bidhaa hiyo ya Mafuta na Gesi.

Balozi Seif alifahamisha kwamba kutokana na thamani kubwa ya bidhaa hiyo katika masoko ya Kimataifa Zanzibar inaweza kupiga hatua kubwa ya Maendeleo na kupunguza tegemezi za mashirika na Taasisi Hisani.

“ Tuna matumaini makubwa kwa Zanzibar kufunguka Kiuchumi kupitia eneo hilo muhimu na kwa vile tayari Viongozi wakuu wa Serikali ya Muungano wa Tanzania kuelezea kwamba hakuna tatizo wala vikwazo kwa Zanzibar la kutaka suala la Mafuta na Gesi kutolewa katika mambo ya Muungano”. Alifafanua Balozi Seif Ali Iddi.

“ Mwaka 2014 hauko mbali kutoka sasa kipindi ambacho tumo katika mchakato wa kupata katiba mpya ya Jamuhuri ya Muungano ambapo wakati huo tutakuwa na uhakika wa kutengamaa kwa suala hilo”. Aliendelea kusisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Ujumbe huo wa Makampuni ya Uwekezaji kutoka Nchini Uholanzi kwamba taratibu za Kisheria zilizopo hivi sasa ndani ya katiba ya Muungano zinaeleza kuwa suala la Mafuta na Gesi ni la Muungano jambo ambalo Zanzibar inahitaji litolewe ili iweze kupata fursa pekee ya maamuzi.

Akizungumzia uimarishaji wa Sekta nyengine za Kiuchumi na Maendeleo Balozi alieleza kwamba lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuimarisha Sekta ya Utalii sambamba na Mipango wa kunanua Bandari ya Malindi ili itoe huduma Kimataifa.

Alisema hatua hiyo itaiwezesha Bandari hiyo kurejea katika Historia na hadhi yake ya kutoa huduma za Kibiashara Kimataifa ndani ya Mwambao wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Akigusia Kilimo Balozi Seif aliuomba Ujumbe huo uliojumuisha pia Wataalamu wa fani tofauti kujaribu kuangalia sekta hiyo ili kuona kama Nchi hiyo inaweza kuisaidia vipi Zanzibar kujiongezea uzalishaji Kitaalamu zaidi.

Alisema wakati Dunia inaendelea kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi wakulima wengi Ulimwenguni wakiwemo wale wa Zanzibar wanaendelea kukabiliwa na Mapato madogo kutokana na ukame unaosababishwa na uchafuzi wa Mazingira.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba mapato ya wakulima wengi yamepunguwa kutokana na uzalishaji mdogo uliokumbwa na mabadiliko hayo ya hali ya hewa.

Mapema Kiongozi wa Ujumbe huo wa Viongozi Wanane wa Makampuni tofauti ya Uwekezaji Nchini Uholanzi Rais wa zamani wa Maseneta wa Bunge la Ulaya Bwana Rene Van Der Linden alisema yapo matumaini makubwa kati ya Uholanzi na Tanzania ya kuendelea kuimarika kwa uhusiano wa pande hizo mbili.

Bwana Rene Van Der alisema ushirikiano wa karibu walioupata kati ya Ujumbe wake na Watendaji wa Serikali zote mbili Nchini Tanzania umefungua ukurasa mpya wa kutanua kwa Miradi ya Pamoja ya Maendeleo na Kiuchumi inayoweza kuekezwe kwa ushirikiano wa sehemu hizo mbili.

“ Tumebahatika kukutana na watendaji wakuu wa Taasisi za Mawasiliano , Maji pamoja na Nishati. Ukweli tumefurahi na tumeanza vyema katika muelekeo wa pamoja”. Alisisitiza Bwana Rene Van Der Linden.

Naye kwa upande wake Balozi wa Uholanzi Nchini Tanzania Dr. Ad Koek Koek alisema Uholanzi imetoa fursa maalum kwa Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na Watendaji na Wataalamu wa Zanzibar kwenda kujifunza Nchini Uholanzi katika masuala ya Mafuta na Gesi.

Dr Ad Koek Koek alisema mpango huo unaweza kusaidia Watendaji na wataalamu wa Zanzibar kupata muelekeo wa Taaluma wakati Zanzibar inaanza na harakati za kuelekea katika miradi mipya katika Sekta ya Mafuta na Gesi.

Balozi Koek Koek aliitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuandaa mpango na ratiba maalum kuhusiana na fursa hiyo kwa ajili ya Wawakilishi, Watendaji na Wataalamu hao kwenda kujifunza Nchini Uholanzi.

Othmana Khamis Ame 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top