Ras Al Khaimah imeshaamua kutoa upendeleo maalum kwa kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika harakati zake za kujiletea Maendeleo ya Kiuchumi, Kijamii sambamba na kupunguza umaskini miongoni mwa Wananchi wake.
 

Mshauri Mkuu wa Mfalme wa Ras Al Khaimah Bwana Salem Ali akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Watano wa Kampuni ya Kimataifa ya Mafuta na Gesi kutoka Nchini humo alisema hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo nyumbani kwake Mtaa wa Farahani Mjini Dodoma.
 

Bwana Salem na Ujumbe wake akiambatana pia na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi na Ushirika Mh. Haroun Ali Suleiman alisema Mpango Maalum ulioandaliwa na Nchi hiyo umelenga kutoa upendeleo kwa Zanzibar kutokana na uhusiano wa Karibu zaidi kati ya Nchi hizo mbili.
 

Alisema mpango huo ambao tayari unatekelezwa katika baadhi ya Mataifa kama Rwanda, Somalia,Pakistan ,Indonesia na Tanzania Bara umelenga kusaidia kuwawezesha Wananchi walio na kipato cha chini ili wafikie hatua ya kujikimu Kimaisha.
 

“ Tumelenga kuwawezesha Wananchi wa kipato cha chini kwa kuwapatia vitendea kazi kama Vyarahani kwa wale wanaotaaluma ya ushoni na Ng’ombe kwa wafugaji wlioko Vijijini”. Alifafanua Mshauri huyo Mkuu wa Mfalme wa Ras Al Khaimah.
 

Bwana Salem Ali alifahamisha kwamba Ras Al Khaimah pia itaendelea kusaidia Zanzibar miradi ya Afya na Elimu ili kuliwezesha Taifa kupata wataalamu zaidi katika masuala ya huduma.
 

Mshauri huyo wa Mfalme wa Ras Al Khaimah Bwana Salem Ali aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano wake na Nchi hiyo ambao amesema ana matumaini kwamba utaendelea kuimarika vyema.
 

Naye Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Mafuta na Gesi ya CEO Rak Gas kutoka Nchini Ras Al Khaimah Bwana Kamal Ahaya alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwamba Uongozi wa Kampuni hiyo uko tayari kuisaidia Zanzibar katika harakati zake za kujinasua Kiuchumi kwa kuunga mkono miradi yake itayoanzisha.
 

Bwana Kamal alisema Kampuni yake yenye uwezo Mkubwa wa Kimataifa katika masuala ya uchimbaji wa Mafuta na Gesi imeshaamua kuipa msukumo Zanzibar kitaalamu itakapofikia hatua ya kuazisha miradi ya mafuta.
 

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliiomba Serikali ya Ras Al Khaimah kupitia Ujumbe wa Viongozi hao kuupa nguvu za ziada mpango huo wa uwezeshaji wananchi hasa Vijijini.
 

Balozi Seif alisema juhudi za Serikali Kuu hivi sasa zimelenga zaidi Vijijini katika harakati za kuwajengea uwezo wananchi wa sehemu hizo ambao ambao ndio wengi katika Jamii.
 

Hata hivyo Balozi Seif alifahamisha kwamba mtazamo zaidi unaendelea kuwekwa katika kukijengea mazingira bora kilimo cha umwagiliaji kwa lengo la kuongeza uzalishaji.
 

Ujumbe huo wa Viongozi wanane wa Kampuni ya Kimataifa ya uzalishaji wa mafuta na Gesi kutoka Nchini Ras Al Khaimah Ukiambatana na Waziri wa Kazi Uwezeshaji Wananchi na Ushirika Mh. Haroun Ali Suleiman ulitembelea Vijiji vya Kiungwi na Mbuyu Tende Kisiwani Pemba katika jitihada za kuangalia namna ya kuwawezesha Wananchi wa Vijiji hivyo Kiuwezeshaji Kiuchumi.
 

Othman Khamis Ame  
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top