Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi Amewataka Vijana wa Jimbo hilo kujiepusha na tabia ya kuwa watoto wa Mitaani na badala yake kushughulikia Taaluma itakayowajengea hatma bora ya maisha yao ya baadae.

Balozi Seif alisema elimu ndio msingi wa Maendeleo ya Mwanaadamu ambayo upatikanaji wake unahitaji juhudi na maandalizi ya pamoja katika Jamii.

Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza hayo hapo nyumbani kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati akizungumza na Vijana 17 wa Kijiji cha Mgambo walioamua kurejea katika masomo yao baada ya kutoroka Skulini kwa kipindi kirefu.

Alisema Watoto wengi Mitaani wanafikia uamuzi wa kuacha masomo yao kutokana na ushawishi wa baadhi ya vigenge vya kihuni vinavyowazunguuka katika maeneo wanayoishi.

Balozi Seif aliwataka Vijana hao kuacha mchezo na kujikita zaidi katika kutafuta Elimu kwani kukimbia Skuli ni sawa na kuyakimbia Maisha mazuri ya Vijana hao hapo baadaye.

Alieleza faraja yake kuona watoto wengi wa Kijiji hicho cha Mgambo wameamua kurejea katika masomo yao baada ya kukaa nje ya Skuli kwa kipindi kirefu.

“ Ukweli nimesikitika sana kuona watoto wengi walioamua kutoroka Skuli wanatoka Kijijini kwangu nilikozaliwa”. Hii inanitia uchungu sana. Alisema Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba si jambo la kawaida kwa Jamii kusimama imara katika kusaidia kuwarejesha masomoni baadhi ya watoto waliotoroka maskulini.

Mapema Msaidizi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi ya Mgambo Ndugu Salim Seif Salim alisema Skuli ya Mgambo hivi sasa inaongoza kwa utoro wa wanafunzi ndani ya Wilaya ya Kaskazini B wanaokadiriwa kufikia hadi watoto 180.

Mwalimu Salim alisema hali ya mazingira ya Kijiji cha Mgambo ya kuwa na vishawishi wingi ndio inayochangia ongezeko kubwa la utoro wa wanafunzi katika Skuli hiyo.

Alifahamisha kwamba Uongozi wa Skuli pamoja na Wazazi imefikia hatua ya kuitumia Kamati ya Polisi Jamii kukabiliana na Watoto wanaozurura Mitaani ili warejee Maskulini.

Kwa upande wake Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi aliwataka Vijana hao kupunguza Vibaraza vinavyochangia watoto hao kujiingiza katika vigenge viovu.

Aliwaasa Vijana hao kutambuja kwamba wao ndio wanaotarajiwa kuwa viongozi watakaoliongoza Jimbo na Kijiji hicho katika maisha ya Jamii itakayowazunguuka hapo baadaye.

Balozi Seif katika kuunga mkono juhudi za Vijana waliowashajiisha Watoto hao kurejea skuli amesaidia Mikoba, Viatu, Mabuku, Sare na Fedha za ushoni kwa Vijana hao 17 ambao baadhi yao wanaonekana kuwa katika mazingira magumu.

Msaada huo wa Mbunge wa Jimbo la Kitope ulikwenda sambamba na kukabidhi Seti ya Jezi na Mipira itakayoendeleza michezo kwa Vijana hao ambao ndio ushawishi Mkuu uliosababisha kurejea tena skulini. Vifaa vyote hivyo vina thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni moja na Nusu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top