Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wivu waliokuwa nao Wananchi wa Vijiji vya Bweleo na Bwefumu viliopo Wilaya ya Magharibi wa kujiletea Maendeleo ndio uliosababisha matatizo yao mwengi kupata ufumbuzi bila ya kutegemea nguvu za wahisani. 

Balozi Seif alisema hayo mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku moja katika Vijiji hivyo kuangalia harakati zao za Maendeleo pamoja na kutambua changamoto zinazowakabili ndani ya Viji vyao. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema mfano huo wa wivu wa Maendeleo ndani ya Bweleo na Bwefumu ambao ni nadra kufanywa na Jamii nyingi alishauri kuwa chachu kwao na Vizazi vijavyo.

Alisema Mataifa mengi Duniani akayatolea mfano wa China na Japani yamefanikiwa kwa kutumia mfumo huu wa kushindana katika maendeleo ndani ya Majimbo na Maeneo yao.

“ Ukiiangalia Jahumuri ya Watu wa China kila Jimbo ndani ya Nchi hiyo imekuwa na shirika lake la ndege kitendo mfumo ambao umesaidia kunyanyuka kwa haraka kwa uchumi wa Mjaimbo hayo na China yenyewe kwa ujumla”. Alisisitiza Balozi Seif.

Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifahamisha kwamba katika kukabiliana na tatizo sugu la ukosefu wa huduma ya Maji safi na salama katika Kijiji cha Bweleo alisema serikali tayari imeshatoa hundi ya shilingi Milioni Hamsini na Nane { 58,000,000/- } kwa ajili ya kuondosha tatizo hilo.

Alisema fedha hizo zimeelekezwa kugharamia kuungwaji wa Mashine na Bomba za maji kutokla Kisima cha Maji kiliopo Dimani ambapo Uongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar umeshaahidi kwamba kazi hiyo itakamilika ndani ya kipindi cha Mwezi Mmoja baada ya kupatikana kwa Feha hizo.

Kuhusu miradi ya Maendeleo ya Vijiji hivyo Balozi Seif katika Kuunga Mkono juhudi za Wananchi hao ameahidi kutoa mchango wa Shilingi Milioni moja { 1,000,000/- } kupiga plasta Jengo la Skuli ya Maandalizi ya Bweleo na shilingi Milioni Moja na Nusu { 1,500,000/- } kukamilisha ujenzi wa sehemu ya kulitia udhu katika Msikiti Kuu wa Ijumaa wa Kijiji cha Bweleo.

Balozi Seif alisisitiza umuhimu wa Elimu na kuwaomba wazazi wa Vijiji hivyo kuendelea kuwekeza Watoto wao katika Sekta ya elimu ambayo ndio itakayowakomboa ndani ya mfumo wa sasa wa Dunia ya Teknolojia.

“ Tumeshuhudia Baadhi ya Wazazi kuwekeza mali zao katika Mashamba, Nyumba na Hata Vipando vya usafiri lakini matokeo yake anaacha vurugu, matatizo kwa kizazi chake wakati wa urithi”. Alifafanua Balozi Seif.

Katika Risala yao iliyosomwa na Mmoja wa Wananchi hao Ndugu Mussa Shaali Choum Wananchi hao walielezea wasi wasi wo kutokana na fujo na vurugu zinazoendelea kutokea katika baadhi ya maeneo hapa Nchini.

Wananchi hao walisema tabia hiyo inayofanywa na baadhi ya Vijana kwa kivuli cha cha Jumuiya ya Uamsho inaleta sura mbaya na ni tabia inayofaa kupigwa vita na jamii yote kwa vile inahatarisha amani ya Nchi.

Katika Ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikagua Skuli ya Bwefumu na kushuhudia baadhi ya majengo ya skuli hiyo yakiwa katika hali ya uchakavu hasa mapaa yake.

Balozi Seif aliuagiza Uongozi wa Jimbo la Dimani kutumia fedha za Mfuko wake wa Jimbo katika kufanya matengengezo ya mapaa ya majengo hayo badala ya kusubiri Wizara husika ambayo imekabiliwa na majukumu manengi.

Balozi Seif pia alikagua eneo la majengo ya Kihistoria ambalo limekuwa na mgogoro wa muda mrefi kati ya Wananchi wa Vijiji hivyo pamoja na Muwekezaji aliyepewa eneo hilo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliahidi kwamba Serikali Kuu itafanya uchunguzi wa kina na baadaye kutoa uamuzi unaostahiki kuhiana na eneo hilo baada ya kujitokeza ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uwekezaji hapa Nchini.

Baadaye Balozi Seif aliangalia Bandari ya Bweleo ambayo Wavuvi wa eneo hilo huitumia kwa shughuli za uvuvi, Mwani pamoja na Kusafirisha Wageni na Watalii kwenda Visiwani.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kijiji hichio Bwana Mataka Makame amemuomba Balozi Seif kwa kuitaka Serikali Kuu kufikiria kuwapatia Vyombo vya Uvuvi pamoja na Vifaa vyake ili kuendeleza kazi zao Bahari Kuu kwa vile eneo la sasa limekuwa na upungufu wa Samaki.

Balozi Seif pia alikaguwa Maendeleo ya Ujenzi wa Skuli ya Maandalizi ya Bweleo, Ujenzi wa Kiwanja cha Kisasa cha Michezo chenye hadhi ya Kimataifa , kuangalisha shughuli za Ushirika wa Akina mama wa Ukweli ni Njia Safi pamoja na Mradi wa Ufugaji Lulu ulio chini ya UItaalamu wa Taasisi ya Sayansi ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam iliyopo Forodhani.

Othman Khamis Ame Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top