Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia maonyesho ya picha katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya mshikamano wa watu wa Palestina yaliyofanyika katika Viunga vya chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } hapo Tunguu Wilaya ya Kati
Juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali ya Misri katika kusaidia mazungumzo ya upatanishi wa kurejea kwa amani ya Mashariki ya Kati na kuzikumba zaidi Nchi za Palestina na Israel imepunguza hali ya wasi wasi na mivutano katika eneo hilo lililotetereka kwa miongo kadhaa iliyopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Mshikamano wa Watu wa Palestina zilizofanyika katika Majengo ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } yaliyopo Tunguu Wilaya ya Kati.
Balozi Seif alisema eneo la mashariki ya kati hasa katika Ukanda wa Gaza na West Banki imekuwa na Historia mbaya ya vurugu na mapambano ya mara kwa mara yaliyosababaishwa na Askari wa Israel dhidi ya Wanamgambo wa Kipalestina.
Alisema kadhia hiyo iliyotoa sura mbaya ya ukatili na udhalilishaji wa Binaadam katika Uso wa Dunia imesababisha kupotea kwa maisha ya Maelfu ya Watu wasio na hatia na wengine kadhaa waliachwa na machungu ya marejaha na Vilema kutokana mivutano hiyo tokea katika miaka ya 60.
Balozi Seif alifahamisha kwamba licha ya mazungumzo mbali mbali na kufikia hatua za kuwekwa saini mikataba iliyosimamaiwa na Mataifa makubwa Duniani lakini bado hali ya mivutano imekuwa ikiendelea kushika kasi kati ya pande hizo hasimu.
“ Tumeshuhudia harakati mbali mbali zilizochukuliwa na Mataifa na Jumuiya za Kimataifa katika kutafuta suluhu ya mivutano ya Mashariki ya kati na hasa Palestina na Israel kwa kufuatiwa na saini za mikataba kama ile ya Camp David Nchini Marekani na ule wa Olso Norway mwaka 1993 lakini hali bado inaendelea kuwa ya wasi wasi”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Mataifa mbali mbali Duniani yanapaswa kusaidia kuipa nguvu Palestina ili ipate kuridhiwa na Umoja wa Mataifa katika maombi yake ya kuwa Taifa huru linalojitegemea.
Aidha amewaomba Wananchi wa Palestina kuzidi kushikamana pamoja katika kutatua kero na matatizo yanayowakwaza katika harakati zao za Maendeleo ikiwa njia ya kukabiliana na change moto zinazowakabili.
Akimkaribisha Makamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ambaye ndie mgeni rasmi Balozi wa Palestina Nchini Tanzania Bwana Nasri Abujaish alisema Wapalestina wanaamini Umoja wa Mataifa bado utaendelea kuwa na dhamana ya kusimamia haki za Wananchi hao wa Palestina.
Balozi Nasri alifahamisha kwamba zaidi ya Wapalestina Milioni 6,000,000 waliyakimbia makazi yao baada ya uvamizi waliofanyiwa mwishoni mwa miaka ya 40 na kusababisha nyumba zao kubomolewa kabisa katika ardhi yao.
Balozi huyo wa Palestina Nchini Tanzania aliyashukuru Mataifa 131 kati ya 193 Wanachama wa Umoja wa Mataifa ambayo yameonyesha dalili za kuunga mkono hatua za Wapalestina za kupigania haki ya kuwa na mamlaka kamili katika Nyanja za Kimataifa.
Balozi Nasir Abujaish ametoa pongezi maalum kwa Tanzania na Zanzibar kwa ujumla kupitia Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } kutokana na juhudi zake za kuiunga mkono Nchi hiyo katika harakati zake za Kimataifa ikiwemo siku hii muhimu ya Maadhimisho ya Kimataifa ya Mshikamano wa watu wa Palestina.
Mapema Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa { UN } anayefanyia kazi zake Tawi la Umoja huo liliopo hapa Zanzibar Bibi Anna Senga amesema Umoja wa Mataifa umekuwa ukipata changamoto kadhaa tokea kuasisiwa kwake.
Bibi Anna Senga alitaja change moto hizo kuwa ni pamoja na matatizo pamoja na mizozo ya Kisiasa Mashariki ya Kati ambayo imekuwa ikichukuwa nafasi kubwa zaidi kwenye majadiliano ya Vikao vya Umoja huo.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata fursa kwa kuzindua maonyesho maalum ya maadhimisho hayo ya siku ya Kimataifa ya Mshikamano wa Watu wa Palestina.
Maonyesho hayo ya picha yamejumuisha baadhi ya harakati za Wapalestina Kisiasa zilizokuwa zikiongozwa na Kiongozi wa kwanza wa chama cha Ukombozi wa Kipalestina { Palestinian Lebaration Organization PLO }.
Othman Khamis Ame. Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top