Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amewataka watendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu Zanzibar kuacha muhali na kufanya kazi kwa uadilifu, ili kuwawezesha wanafunzi wenye sifa kupatiwa mikopo hiyo.

Amesema lengo la serikali kuanzisha bodi hiyo ni kuwawezesha watoto wa kimaskini kuweza kujiendeleza kielimu kwa kupatiwa mikopo, na wala sio kuwakopesha watoto wa viongozi ambao wazee wao wanaweza kuwalipia.

Maalim Seif ametoa changamoto hiyo leo wakati alipotembelea ofisi za bodi hiyo zilizopo Mnazimmoja ikiwa ni mfululizo wa ziara yake ya kutembelea taasisi za elimu nchini.

Aidha ameitaka bodi hiyo kufanya kazi kwa uwazi na kuwaelimisha wananchi juu vipaumbele na uwezo wa bodi hiyo, ili kuondosha malalamiko yanayojitokeza mara kwa mara.

Amesema bodi hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wenye sifa wanapatiwa mikopo kwa ajili ya kujiendeleza kitaaluma, licha ya kuwa na uwezo mdogo wa kifedha kulingana na mahitaji ya wanafunzi, jambo ambalo linapaswa kufanywa kwa uadilifu.

Amefahamisha kuwa serikali kwa upande wake imejitahidi kuongeza bajeti ya bodi hiyo kwa asilimia mia moja katika mwaka huu wa fedha wa 2012/13 kutoka shilingi bilioni 4 hadi bilioni 8.

Makamu wa Kwanza wa Rais amepongeza hatua ya bodi hiyo ya kutaka kuanzisha maombi ya mikopo kupitia njia ya mtandao “Application on line”, hatua ambayo itawarahisishia wanaoomba mikopo hiyo pamoja na bodi yenyewe.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa bodi hiyo bwana Iddi Khamis Haji amesema bodi imekuwa ikijitahidi kutoa mikopo hiyo kwa kuzingatia vipaumbele vya serikali, lakini imekuwa ikipokea malalamiko kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaoomba mikopo ambapo uwezo wa bodi hiyo bado ni mdogo kuweza kuwapatia wanafunzi wote.

Amefahamisha kuwa katika mwaka huu wa masomo bodi imeweza kuwapatia mikopo wanafunzi 800 tu ambapo wenye sifa ya kupatiwa mikopo hiyo walikuwa 1800, na kuongeza kuwa bodi yake imelazimika kusitisha kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaoomba kusoma nje ya nchi kutokana na gharama kubwa.

Katika hatua nyengine Makamu wa Kwanza wa Rais amepongeza mafanikio yaliyopatikana katika Chuo Kikuu Kishiriki Cha Elimu Chukwani, na kwamba mafanikio hayo ni kielelezo cha mchango mzuri wa sekta binafsi katika mfumo wa elimu nchini.

Miongoni mwa mafanikio ya chuo kicho ni kuwepo kwa kiwanda kikubwa cha uchapishaji “Press” ambacho kimekuwa kikitoa huduma hata kwa taasisi za serikali, pamoja na kuongeza programe zake kutoka zile za masomo ya Elimu ya Dini ya Kiislamu na Kiarabu. Kwa sasa chuo hicho pia kinafundisha masomo ya sayansi na kompyuta kwa ngazi ya shahada ya kwanza.

Mkuu wa Chuo hicho Dr. Hamed Rashid Hikman amesema tayari masuala ya usajili yameshaanza katika kukifanya chuo hicho kuwa chuo kikuu kamili.

Dr. Hikman amefahamisha kuwa chuo hicho pia kina mpango wa kuanzisha maabara ya lugha pamoja na kituo cha matangazo kwa kushirikiana na baadhi ya vituo vya matangazo ili kuwawezesha wanafunzi kuweza kujifunza kwa urahisi.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Kiislamu Mazizini Dr. Muhidini Ahmed Khamis ameiomba serikali kutekeleza azma ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ya kukifanya chuo kikuu, pamoja na kulinda uvamizi wa eneo hilo la chuo.

Akizungumzia kuhusu migogoro ya Ardhi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Ali Juma Shamuhuna amesema wanakusudia kulivalia njuga suala hilo ili kuhakikisha kuwa ardhi katika taasisi za elimu haiporwi tena.

Katika ziara hiyo iliyomuhusisha pia Naibu Waziri Mhe. Zahra Ali Hamad, walitembelea Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Mbweni. 
Hassan Hamad (OMKR).

0 comments:

 
Top