Uturuki inakusudia kutoa upendeleo Maalum kwa Zanzibar ili kusaidia Taaluma na baadhi ya Uwezeshaji katika Sekta za Utalii na Biashara lengo likiwa ni kuimarisha Mapato ya Serikali pamoja na kunyanyua ustawi wa Wananchi ambao hutegemea Sekta hizo Kimaisha.

Waziri wa Chakula, Kilimo na Mifugo kutoka Nchini Uturuki Bwana Mehdi Eker alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Mehdi Eker ambae yupo Zanzibar kwa ziara ya Kiserikali ya Siku mbili akiuongoza ujumbe wa Viongozi 20 waosimamia Sekta hizo mbili alisema kwamba Uturuki iko tayari wakti wote kuugawa Utaalamu iliyokuwa nao kwa ndugu zao wa Zanzibar.

Waziri Mehdi alisema utaratibu maalum unapaswa kuandaliwa kwa kuyatumia mabaraza ya Ushirikiano yanayohusika na masuala ya Biashara ya pande hizo mbili katika kupanga mikakati ya kufanikisha mpango huo muhimu.

Bwana Mehdi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba katika kuendelea kuimarisha uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya Uturuki na Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa ujumla alisema Mpango huo ni vyema ukaenda sambamba na kujumuishwa kwa Ushirikiano wa Sekta nyengine katika hatua za baadaye.

Alizitaja baadhi ya sekta hizo muhimu kwa uchumi wa pande hizo mbili kuwa ni pamoja na Nishati, Madini, Kilimo , Ujenzi sambamba na kushirikishwa kwa sekta Binafsi ambazo zinasehemu kubwa ya kuchangia Uchumi huo.

Akizungumzia Sekta ya Utalii Waziri wa Chakula, Kilimo na mifugo wa Uturuki Bwana Mehdi Eker alieleza kwamba Zanzibar inaweza kulitumia soko la Utalii la Uturuki katika kuimarisha Uchumi wake.

Alimueleza Balozi Seif kwamba Uturuki kwa kutumia Mji Mkuu wake wa Istanmbul imekuwa Kituo kikuu cha harakati za Utalii kati yake na Nchi za Ulaya kupitia Uholanzi kwa kipindi kirefu sasa.

“ Mji wa Uturuki wa Istanmbul umekuwa maarufu sana kwa shughuli za Kitalii ikiwa ni kiungo mama na Nchi wa Bara la Ulaya kwa kupitia Amsterden Nchini Uholanzi kwa zaidi ya miaka 400 iliyopita”. Alifafanua Waziri Mehdi.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Serikali ya Uturuki kwa hatua yake kubwa iliyopiga katika kujiletea maendeleo ambayo tayari imeshaonyesha nia sahihi ya kutaka kuchota maendeleo hayo kwa ajili ya kuipatia Zanzibar.

Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshajizatiti kuona Sekta ya Utalii inaimarika vyema juhudi ambazo zilianza katika miaka ya 80 baada ya zao tegemezi la Uchumi wa Zanzibar ambalo ni Karafuu kuonekana likiyumba katika soko la Kimataifa.

Hata hivyo Balozi Seif alimueleza Waziri wa Chakula, Kilimo na Mifugo wa Uturuki kwamba Serikali pia inaendelea na jitihada za kuimarisha miundo mbinu katika dhana ya kuzijengea uwezo sekta nyengine muhimu kwa maslahi ya Jamii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliiomba Uturuki kuangalia uwezekano pia wa kusaidia Taaluma katika kilimo cha umwagiliaji kwa lengo la kuwawezesha wakulima kupata chakula cha kutosha.

Alisema juhudi za ziada zinahitajika kuchukuliwa kitaalamu katika kuona ardhi ndogo iliyopo hapa Zanzibar inatumiwa vyema na kwa uangalifu wa hali ya juu.

Othman Khamis Ame 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top