Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeombwa kufikiria muundo wa Miradi mbadala ya Kiuchumi itakayosaidia kutoa ajira, kulinda Mazingira ya Bahari pamoja na kupunguza msongamano wa wavuvi katika Ghuba ya Chwaka na Marumbi.
Muundo huo wa miradi Mbadala kwa njia nyengine pia utakuwa suluhisho la kudumu
la mgogoro wa muda mrefu wa uvuvi unaokaribia miaka 35 sasa kati ya
Vijiji jirani vya Chwaka na Marumbi viliopo Wilaya ya Kati.
Ombi hilo limetolewa na Wananchi wa Kijiji cha Chwaka wakati wakitoa kero pamoja na
changamoto zinazowakabili mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi hapo katika uwanja wa soka wa Chwaka Wilaya ya
Kati.
Mkutano
huo wa Balozi Seif ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa wakati
alipokutana na Wananchi wa Marumbi kupokea kero na Matatizo yao miezi
michache iliyopita ambayo yanavihusu Vijiji hivyo kwa pamoja kubwa hasa
ni suala la Uvuvi.
Bwana Vuaa
Mwadini Mcha alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba idadi
kubwa ya Wavuvi wanaofanya shughuli zao za Uvuvi katika ghuba ya Chwaka
imekuwa kubwa kulinganisha na uwezo wa ghuba yenyewe.
Hata
hivyo Bwana Vuaa alisema Wananchi wa Chwaka wako tayari wakati wowote
kumeguka kwa asilimia kubwa kutoka katika shughuli za Uvuvi kama
Serikali itaanzisha miradi ya Kiuchumi itakayowawezesha Wananchi hao
kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao ya kila siku.
“
Tunakumbukumbu nzuri tusiyoisahau ya Rais wa Awamu ya Pili Mzee Aboud
Jumbe Mwinyi wakati ule alipotutaka tuachane na uvuvi wa juwa. Kwanza
alituwezesha kwa kutuletea nyavu na baadaye taaluma ya matumizi bora ya
Bahari mpango ambao ulifanikiwa kwa kiwango kikubwa sana”. Alifafanua
Bwana Vuaa Mwadini.
Alimuhakikishia Balozi Seif kwamba Wananchi na Wavuvi wa Chwaka hawana ugomvi na Wananchi wa Marumbi lakini kinachojitokeza ni Baadhi ya Viongozi wa Serikali na Polisi Wilaya ya Kati kuwa na kigugumizi cha kuchukuwa hatua za kisheria wakati yanapotokea matatizo hasa ya Uvuvi baina ya pande hizo mbili.
“ Chwaka haiko tayari Mwananchi ye yote afariki kutokana na ugomvi wa Uvuvi. Lakini tumefikia wakati kukosa imani dhidi ya uongozi wa Polisi na Serikali wa Wilaya ya Kati kwa kushindwa kuchukuwa hatua za kisherika kwa watu wanaokiuka sheria hizo.
Naye
Bwana Nuru Muhammad alielezea masikitiko yao kutokana na Mradi mkubwa
ulioanzishwa chini ya uhadhili wa Benki ya Dunia wa kuwawezesha wavuvi
wa Ghuba hiyo { Macemp } kutowanufaisha Wavuvi hao ambao ndio walengwa
wa mradi huo.
Bwana Nuru alifahamisha kwamba licha
ya juhudi zilizochukuliwa na Wawakilishi wa Mradi huo kupitia
wasimamizi wa Benki ya dunia wa kukutana na Wananchi hao kwa kupanga
malengo ya mradi huo kiutekelezaji kwa vile mfuko wa mradi huo haukuwa
na mashaka lakini kilichojichomoza zaidi kwa mfuko huo ni kuendelezwa
kwa semina na vikao.
“
Inasikitisha kuona Vikao mbali mbali vilifanywa kwa kushirikishwa
wavuvi husika lakini nguvu za mradi huo zikaelekezwa sehemu nyengine
bila ya kuwanufaisha walengwa ambao ni sisi Wavuvi”. Alisisitiza Bwana
Nuru.
Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wajibu wa Serikali wakati wote ni kufuatilia na kujua kero zinazowakabili Wananchi na kuzitafutia ufumbuzi unaostahiki.
Balozi Seif alielezea kusikitishwa kwake na mgogoro wa uvuvi unaotia doa mfumo wa amani na utulivu Nchini unaovikumba Vijiji vya Chwaka na Marumbi kwa karibu miaka 35 sasa.
“ Sisi tunataka amani na utulivu, watu waishi pamoja, wafanye kazi pamoja, haya mambo ya Ukafu na
uccm hayana nafasi tena katika Jamii. Tunachokizingatia zaidi kwetu
sisi kama Serikali ni kuona wananachi wanaishi kwaamani na kushirikiana pamoja”. Alisisitiza Balozi Seif.
Katika Mkutano huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliahidi kutoa Mabomba 800 pungufu yaliyooelezwa ndani ya risala ya Wananchi hao wa Chwaka kukamilisha Mabomba 1200 yaliyokisiwa kutumika katika mradi wa Maji safi na Salama katika Shehia hiyo.
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Mh. Ramadhan Abdulla Shaaban aliahidi kugharamia ujenzi wa Tangi la Maji ili kukamilisha mradi huo muhimu.
Hata hivyo Waziri Shaaban aliwanasihi Wananchi hao wa Chwaka kuwa na stahamala kidogo kwa vile kazi hiyo inahitaji gharama ambayo kwa hivi sasa itahitajika kutafutiwa bajeti yake.
Aliwataka Wananchi hao wa Chwaka kuwa tayari wakati utapowadia kuitekeleza kazi hiyo kwa ushirikiano na Watendaji wa Taasisi za Wizara hiyo kwa njia ya mpango wa ujenzi wa Taifa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu Pili wa Rais wa
Zanzibar
0 comments:
Post a Comment