WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa wanapofanya uchaguzi wa viongozi lazima wazingatie aina ya viongozi wanaohitajika kwa kuendelea kulinda Taifa, heshima na majukumu ya chama hicho huku wakitambua kuwa Sera ya CCM ni Muungano wa Serikali mbili.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  aliyasema hayo leo katika Mkutano wa uchaguzi wa CCM Mkoa wa Mjini katika hotuba yake kwa wanaCCM pamoja na Wajumbe wa Mkutano huo huko katika Afisi za CCM Mkoa wa Mjini, Amani Zanzibar.
Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein alisema kuwa CCM inahitaji viongozi wenye uwezo, uwadilifu na wanaowanganisha wanachama katika ngazi mbali mbali sambamba na kuwa na uwezo wa kuieleza, kuitetea na kuisimamia Ilani ya CCM ya mwaka 2010.
Alisema kuwa kila mmoja anaelewa kwamba kuongoza ni kuonesha njia na ili kiongozi aweze kuongoza vyema, inabidi aelewe,aikubali na aitekeleze kwa vitendo misingi ya chama hicho.
Dk. Shein alisema kuwa kiongozi wa CCM hana budi kutembea kifua mbele na kujivunia mafanikio yaliyoletwa na Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 kwa kuwaletea wananchi hali bora ya kiuchumi na ustawi wa jamii.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa jambo la msingi ni kuendeleza Muungano ulioasisiwa tarehe 26 Aprili, 1964 na kueleza kuwa Sera za CCM ziko wazi juu ya aina ya Muungano ambao utaendelea kuwa imara.
“Sera ya CCM imeweka bayana mfumo wa Serikali mbili katika Muungano wetu na kila kiongozi wa CCM anapaswa kulikubali hilo na kutolionea haya kwa kulisema wazi wazi bila ya kutafuna maneno. Mifumo mengine haitokani na Sera za Chama Cha Mapinduzi”,alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa ingawa vyama vikuu vya siasa hapa Zanzibar vinashirikiana katika Serikali kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Toleo la 2010 lakini kila chama kina sera yake, Katiba yake, ratiba zake na taratibu zake.
Dk. Shein aliwataka wana CCM kuendelea kuimarisha amani na utulivu kwa vitendo na kuendelea kufanya siasa katika mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa kuzingatia sheria na taratibu ziliopo na kuwataka kuwa imara kwani wanaongozwa na viongozi imara na wenye busara.  “Tuwe wavumilivu na wastahamilivu kwani uvumilivu na ustahamilivu sio udhaifu bali ni njia ya uungwana katika maisha ya kila siku”,alisisitiza Dk. Shein.
Katika hotuba yake hiyo pia, Dk. Shein aliewaeleza Wana CCM hao watambue kuwa chama hicho kinaendeleza siasa ya msingi ya ujamaa na kujitegemea, wala wasidhani kama CCM imebadilisha hilo.
Alisisitiza kuwa CCM ni chama kikongwe hivyo ni wmalimu wa siasa kwa vyama vyengine vya siasa hapa nchini na kutokana na hilo ni lazima chaguzi zao zitoe darasa la ukomavu wa demokrasia ndani ya vyama vya siasa.
Dk. Shein aliwataka wale wote waliokwisha chaguliwa na watakaochaguliwa waelewe kwamba wameaminiwa hivyo ni lazima waoneshe imani kwao  na wajue kuwa hiyo ni changamoto kwao hivyo wanapaswa kutekeleza dhamana walizoziomba.
Alieleza kuwa uchaguzi wa viongozi ni hatua muhimu ya kupanga safu ya uongozi ikitiliwa maanani kwamba chama hicho kinakabiliwa na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, hivyo katika hali kama hivo ni lazima wajipange vizuri tena kwa uhakika na sio mzaha.
Aliwataka viongozi watakaopewa dhamana ya kuitumikia CCM, wanachama na wapenzi wa chama hicho lazima wawe tayari na wawe mstari wa mbele kuyatangaza mafanikio yaliokwisha patikana katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010-2015.
Pia aliwasihi waliogombania nafasi wawe tayari kuyapokea matokeo yoyote kwa sababu zaidi ya hayo atowae uongozi ni Mungu na kiongozi huwekwa na MwenyeziMungu.
Mapema Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini Alhaj Mwangi Kundya aliahidi kuwa uchaguzi huo utaenda vizuri na watachaguliwa viongozi wa kuonesha njia.
 Alhaj Kudya kwa niaba ya wanaCCM alieleza imani yao kubwa kwa Dk. Shein kutokana na juhudi zake tokea alipoingia madarakani kwani wamekuwa wakivutiwa na hatua za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein.
Alieleza mafanikio yalipatikana katika miradi ya maendeleo ukiwemo utalii, hatua za ongezeko la bei ya karafuu, kupunguza bei ya pembejeo za kilimo, mashine mpya za kuvunia mpunga pamoja na kuzindua mradi mpya wa umeme hapo majuzi. 
Wakati huo huo, Dk. Shein alikwenda kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua Viongozi wa  ngazi mbali mbali za Mkoa Mpya wa CCM Magharibi, huko katika kituo cha Chuo cha Ufundi Karume, kiliopo Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

0 comments:

 
Top