Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri
Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi amekemea tabia ya
baadhi ya Wana CCM kuachana na tabia ya kujijengea mazingira ya kukiona chama
hicho kizuri wakati wanapokuwa madarakani
tu.
Alitoa kemeo hilo wakati akiufungua
mkutano Mkuu wa uchaguzi CCM wa Mkoa wa Kusini Unguja hapo katika ukumbi wa Tamarind
Beach Hotel iliyopo Uroa Mkoa wa Kusini Unguja.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar alisema tabia hiyo inayoonekana kuanza kuchipua ndani ya Chama ni
ya hatari na inafaa Viongozi kama hao wakaepukwa
kabisa.
Alisema Chama cha Mapinduzi hakiwezi
kuendelea kuwa na makundi ya wanachama ambayo hatimae husababisha mvutano wa
Viongozi na hatiae kushindwa kutetea na kulinda Sera za Chama hicho.
Alitahadharisha kwamba Viongozi wanaoweka
maslahi mbele ndio wenye hulka ya
kuogolea zaidi katika rushwa inayopigwa
vita na kukemewa kabisa ndani ya sera na ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Alionya kuwa uongozi hauombwi kwa
rushwa na kuwataka wanachama kuwakimbia watu wanaoendeleza tabia hiyo ambayo ni
mbaya kabisa inayoweza kuwajengea muelekeo mbovu wa chama hicho.
Balozi Seif alisisitiza kwamba katika kukabiliana na tatizo la rushwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuunda chombo kitakachokuwa na
uwezo wa kusimamia udhibiti wa rushwa ili kupunguza au kuondosha dhambi hiyo
mbaya.
Balozi Seif alitoa mfano wa Kiongozi
bora ni yule anayejiamini kwa kutumia nguvu, busara na hekima katika kuwaongoza
wanachama na Jamii iliyomzunguuka.
“ Wapo baadhi ya wanachama wenye tabia ya
Mchwa ndani ya Chama ambao huitafuna
miradi kadhaa ya chama hicho ambayo inauwezo kabisa ya kukiendesha chama
kiuchumi”. Alifafanua Balozi Seif.
Akizungumzia suala la demokrasia
nchini Balozi Seif alisema fursa hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya na baadhi ya
watu na hata vikundi vya dini kwa kuilazimisha jamii au wafuasi wao kufuata
yale matakwa wanayoyahitaji bila ya kuzingatia uhuru wa mtu.
Alisema tabia hiyo haitoi ile haki halisi ya Demokrasia inayohitajika ambayo ipo kwa mujibu wa Katiba na Sheria za
Nchi.
“ Kwa nini leo Demokrasia ipo tena ndani ya vyama vya siasa na hata katika Taasisi
za Kijamii halafu wanakuwepo baadhi ya watu au vikundi vya jumuiya za Kiraia zilazimishe
yale wanayoyataka wao tena kwa nguvu ?”. Alihoji Balozi Seif.
Aliwapongeza Wananchi wa Mkoa wa
Kusini Unguja kwa kupitisha mchakato wa katiba mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa njia ya amani na usalama.
Mapema akimkaribisha Balozi Seif
Mwenyekiti wa CCM aliyemaliza kipindi cha miaka mitano iliyopita Mkoani humo
Ndugu Haji Ussi Gavu alisema Mkoa wa Kusini Unguja umepata Heshima kubwa ndani
ya Mikoa yote ya Tanzania Kisiasa.
Ndugu Gavu alisema heshima hiyo imekuja
kutokana na umadhubuti wa wanachama na Viongozi wa Mkoa huo uliopelekea kuwa
ngome imara ya Chama cha Mapinduzi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
0 comments:
Post a Comment