RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amekabidhiwa ripoti ya kuzama kwa Meli ya MV Skagit na Tume ya Uchunguzi wa ajali hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Jaji Abdulhakim Ameir Issa. 
Mara baada ya kupokea ripoti, Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa Tume hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya na hatimae kuandaa ripoti hiyo iliyotoa taarifa juu ya ajali ya kuzama kwa meli ya MV Skagit na kueleza kufarajika kwake kutokana na kutumia muda mfupi wa kuwasilisha ripoti hiyo.
Dk. Shein alisema kuwa jitihada za makusudi zitachukuliwa na Serikali katika kuhakikisha mapendekezo yote yaliotolewa katika ripoti hiyo yanatekelezwa kikamilifu na kufanyiwa kazi ipasavyo kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi ziliopo.
Alisema kuwa kufanikiwa kwa ripoti hiyo ambayo imechukua muda mfupi imetokana na uzoefu mkubwa wa Tume hiyo kutokana na Tume hiyo kufanya kazi kama hiyo kwa ufanisi zaidi baada ya kuiteua kufanya kazi ya kuzama kwa Meli ya MV Spice Islander mwezi Septemba mwaka jana.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisisitiza kuwa kutokana na uzoefu huo ndio sababu kubwa iliyompelekea kuiteua tena Tume hiyo kwa kufanya kazi hiyo ambayo hatimae imekabidhisha ripoti yake kwa wakati muwafaka.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na mashirikiano makubwa yaliopo ndani ya Tume hiyo na kuwataka kuongeza zaidi ushirikiano huo katika kazi zao za kila siku.
Dk. Shein aliahidi kuwa taarifa zaidi zitatolewa kwa wananchi juu ya uchunguzi huo kwa uwazi pamoja na hatua zitakazochukuliwa na serikali sambamba na kuiweka ripoti hiyo kwenye mtandao kwa lengo la kuwapa taarifa za uhakika wananchi.
Alisisitiza kuwa ripoti hiyo itafanyiwa kazi na serikali kwa kuzingatia haki na uadilifu pamoja na kuzingatia Kaatiba ya Zanzibar, Sheria na taratibu za nchi zilizopo.
Mapema  Mwenyekiti wa Tume hiyo ya Uchunguzi wa kuzama kwa Meli ya MV Skagit Mhe. Jaji Abdulhakim Ameir Issa alimueleza Dk. Shein kuwa Tume hiyo iliyoanza kazi zake Agosti 1, 2012 na kumaliza Septemba 15, mwaka huu imefanya kazi zake vizuri kwa kupata mashirikiano kutoka kwa wahusika mbali mbali.
Alisema kuwa Tume hiyo iliyokuwa na wajumbe 10 ilipita katika maeneo mbali mbali ya Unguja, Pemba na Dar-es-Salaam wakati wakikusanya taarifa za ripoti hiyo na kuweza kupata mafanikio.
Mwenyekiti huyo alimueleza Rais sababu zilizopelekea kuzama kwa meli hiyo pamoja na mapendekezo ya Tume hiyo iliyoyapendekeza.
Tume hiyo iliteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein tarehe 23 Julai mwaka huu ambayo wajumbe wake ni Mwenyekiti Jali Abbdulhakim Ameir Issa, Katibu wake Shaaban Ramadhan Abdalla.
Wengine ni Salum Toufiq Ali, Kepteni Hatib Katandula, Bi Mkakili Fausta Mbowi, Komodoo Hassan Mussa Mzee, Meja Jenerali S.S. Omar, Kepteni Abdalla Yussuf Jumbe, Kepteni Juma Abdalla na Bwana Omar Chengo.
Akitoa neon la shukurani kwa niaba ya Tume hiyo Bwana Omar Chengo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa ni imani yao kubwa kuwa wamefanya kazi vizuri tena kwa ufanisi mkubwa.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, ajali ya kuzama kwa meli ya MV Skagit  ilitokea Julai 18 mwaka huu mnamo majira ya saa 7:30 za mchana, wakati meli hiyo ikitokea Dar-es-Salaam kuja Zanzibar ikiwa na abiria 447 pamoja na mizigo kadhaa ya abiria.
Ambapo alieleza kuwa katika ajali hiyo watu 212 wamepotea na watu 154 walinusurika na waliokufa walifikia idadi ya 81 wakiwemo Watanzania 75, Wakenya 3, Waholand 2 na Mrundi 1.
   Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

0 comments:

 
Top