Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
haitamuonea haya wala kumuogopa mtu ye yote ambae atabainika kuhusika na uvunjifu wa amani
baada ya Seriikali kuvumilia vya kutosha, uvumilivu ambao umefikia kikomo.
Kauli hiyo imetolea na Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiufunga mkutano wa Tisa wa
Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa
ukifanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema Serikali kupitia
vyombo vya ulinzi itaendelea kuvisaka vikundi vya kihuni vinavyoendesha vitendo
vya kuwatisha Wananchi na kuwanyang’anya vitu na mali zao, kuchoma moto baadhi
ya Majengo sambamba na kuharibu miundo mbinu ya Bara bara.
Alisema hali hiyo ya vurugu sio Utamaduni wa Wananchi
wa Visiwa hivyi ambayo ni ya kusikitisha iliyopelekea wananchi kuacha shughuli
zao za kujitafutia riziki kutokana na kusimama kwa harakati zao za maendeleo
“ Tutafanya kosa kubwa sana ikiwa tutaanza kuichezea amani
tuliyonayo kwani kuvunjika kwa amani Nchini mwetu ndio chanzo cha kuvunjika kwa
Umoja wetu.” Alisisitiza Balozi Seif.
Aliwanasihi Wananchi kuacha
kujiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani kwani kutenda hivyo ni kosa kwa
mujibu wa sheria na Serikali haitasita kumchukulia hatua mtu ye yote
atakayejihusisha na vitendo hivyo.
Aidha Balozi Seif aliwaomba Wananchi
kutoa Taarifa kwa vyombo vya dola mara tu watakapoona dalili za watu wenye nia
ya kutaka kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
Akizungumzia suala la Rushwa Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali inaendelea kuchukuwa
hatua za kuimarisha Taasisi za kupambana na Rushwa.
Alisema Viongozi pamoja na Wananchi
wana wajibu wa kutoa ushirikiano kwa
Taasisi ya kupambana na Rushwa iliyopitishwa na Baraza hilo hivi karibuni ili
iweze kutekeleza majukumu na wajibu wake
kwa mujibu wa sheria na kwa kwa faida ya maendeleo ya Taifa.
“ Kama sote tunavyojua rushwa ni adui
wa haki na hivyo haina budi kupigwa vita ili itokomezwe kabisa. Lakini hizi
hazitafanikiwa bila ya ushirikiano wa wananchi wenyewe”. Alifafanua Balozi
Seif.
Kuhusu kundi la watu wenye Ulemavu
Balozi Seif alisema Serikali imeweka mikakati katika kujenga usawa na kuheshimu
haki za watu wote wenye ulemavu.
Alieleza kwamba kuwapatia watu wenye
nulemavu haki zao za msingi ni jambo la Kikatiba na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar itahakikisha azma hii inafikia malengo yaliyowekwa.
Balozi Seif aliipongeza Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa juhudi kubwa inayochukuwa katika
kuimarisha mazingira kwa watu wenye ulemavu na kuwajengea uwezo wa kushiriki
katika maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi.
Akigusia suala la tume ya kukusanya
na kuratibu Maoni ya Mabadiliko ya Katiba ya Muungano Balozi Seif aliwaomba
Wananchi ambao bado hawajatoa maoni yao kuitumia fursa hiyo itakayoamua mambo
muhimu yatakayokuwa na maslahi kwa Jamii yetu.
Alisema si vyema kwa baadhi ya
vikundi vya Wananchi kuiacha fursa hii na kuendelea kutoa matamshi
yanayochochea nchuki, uhasama na vurugu kwa kisingizio cha kuukataa Muungano.
ASlisisitiza kwamba jambo la kubwa la kuzingatia ni kuitumia fursa hii ili
Wananchi wote waweze kuitoa maoni yao kwa uhuru bila ya kubughudhiwa na
kutishiwa maisha yao.
Kuhusu Sekta ya Umeme Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar alisema suala la
mgao wa umeme karibu litakuwa historia katika Kisiwa cha Unguja kufuatia
kutandikwa kwa waya mpya wa umeme wenye uwezo wa kuchukuwa umeme wa Mega Watts
100 kazi ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi Disema mwaka huu wa 2012.
Alisema hatua hii ni faraja kubwa kwa
Wananchi wa Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba umeme ndio nishati muhimu kwa
shughuli za uzalishaji na maendeleo ya Taifa hili.
Aliwataka Wananchi wote waendelee
kuitumia nishati ya umeme kwa shughuli zao za kujiajiri kwa nia ya kujikomboa
kutoka kwenye umaskini.
Baraza la Wawakilishi Zanzibar
limeahirishwa hadi jumatano ya Tarehe 16
Januari mwaka 2013 saa 3.00 za Asubuhi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
0 comments:
Post a Comment