Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi alisema ipo haja kwa jumuiya za Kitaifa na Kimataifa kuendelea
kujaribu kuipa msukumo Michezo inayoonekana
kuwa sio maarufu ili ipate nguvu
za ziada kutokana na umuhimu wake ndani ya Jamii.
Alisema michezo imekuwa nyenzo muhimu
inayosaidia kuipatia umaarufu Nchi inapoamua kuimarisha sekta ya michezo na hatimae kupelekea
kuongezeka kwa mapato ya Taifa kunakotokana na muingiliano wa wageni kupitia
sekta hiyo.
Balozi Seif alieleza hayo hapo
Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar mara baada ya kupokea ripoti ya Mpira wa wavu
wa Ufukweni Zanzibar { Beach Volley Ball } kutoka kwa Ujumbe wa Chama cha
Mchezo huo ukiongozwa na Rais wake Bwana Saleh Salim Saleh.
Amefahamisha kwamba Zanzibar
ilibahatika kupata sifa nyingi ndani ya ramani ya Dunia kupitia sekta ya
Michezo katika miaka ya nyuma lakini hivi sasa sifa hiyo imetoweka baada ya
Michezo kadhaa kufifia na mengine kufa kabisa.
“ Tumeshuhudia enzi zetu wakati
tukishiriki michezo tofauti umri ambao tulikuwa maskulini hali iliyopeleka
miongoni mwetu kuiiwakilisha Nchi katika michezo ya Kimataifa. Utaratibu huo
kwa sasa umetoweka Maskulini sasa tutarajie nini? “. Aliuliza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Chama cha Mpira wa Wavu wa Ufukweni Zanzibar
kwa uwamuzi wake wa kuanzisha Mchezo huo hapa Nchini.
Alisema Mchezo wa Wavu wa Ufukweni
unaonekana kupendwa sana na wageni pamoja na Watalii, hivyo kuanzishwa kwake
hapa Nchini kutasaidia kwenda sambamba na ile dhana ya Serikali ya kuwa na
Mpango wa Utalii kwa wote.
Balozi Seif alitoa wito kwa washirika
wa Michezo ndani na nje ya Nchi kutoa
msukumo kwa mchezo huo ili ile azma ya kuanzishwa kwake iweze kufikiwa vyema.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
alifahamisha kwamba kwa vile mchezo huo huchezwa zaidi katika maeneo ya futwe aliutahadharisha
Uongozi wa Mahoteli yaliyoko karibu na Fukwe hizo kutowazuia wanamichezo hao
kufanya mazoezi yao.
Balozi Seif alieleza kuwa Vitendo hivyo kama vinafanywa
na baadhi ya Mahoteli hayo waelewe kwamba kufanya hivyo ni kwenda kinyume na
utaratibu wa matumizi ya fukwe hizo.
“ Upo utaratibu uliowekwa na Serikali
kupitia Taasisi ya uwekezaji Vitega uchumi Zanzibar { ZIPA } kuwataka wawekezaji wote wanaowekeza
Vitega Uchumi vyao katika maeneo ya karibu na Bahari kuheshimu Mita 30 za fukwe
ili kulinda mazingira”. Alifafanua Balozi Seif.
Akisoma Ripoti hiyo Mwenyekiti wa Chama wa Mpira wa Wavu wa Ufukweni Zanzibar
{ ZBV } Bibi Mwanaisha Saidzain Abubakar alisema lengo la kuanzishwa kwa mchezo
huo hapa Nchini ni kuitangaza Zanzibar
Kitaifa na Kimataifa.
Bibi Mwanaisha aliyataja malengo
mengine kuwa ni pamoja na kukuza na kuendeleza michezo, kutafuta vipaji vya
wachezaji, kuitangaza Zanzibar kiutalii kupitia mchezo huo pamoja na kubuni
ajira kwa Vijana.
Mwenyekiti huyo wa Chama cha Mpira wa Wavu wa Ufukweni
Zanzibar alisema mchezo wao umekuwa ukikabiliwa na changa moto zinazopeleka
kuwaweka katika mazingira magumu kimazoezi na hata mashindano.
Bbibi Mwanaisha alizitaja baadhi ya
changa moto hizo kuwa ni pamoja na
ukosefu wa viwanja vya mazoezi, Vifaa vya michezo, wafadhili pamoja na
ukosefu wa fedha wakati wa kuandaa mashindano yanayokwenda sambamba na utowaji
wa elimu.
Naye kwa upande wake Rais wa Chama
cha Mchezo wa Wavu wa Ufukweni Bwana Saleh Said Saleh alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar kwa juhudi zake za kusimamia maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar akiwa
Mtendaji Mkuu wa Serikali.
Chama cha Mchezo wa Wavu wa Ufukweni
Zanzibar {Beach Volley Ball } kimezindua mchezo huo hapa Zanzibar Mwezi Febuari
Mwaka huu kwa kuandaa mashindano yaliyoshirikisha Timu saba za Mchezo huo ambazo zilizojumisha
Timu za Vikosi vya Ulinzi na zile za Kiraia.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
0 comments:
Post a Comment