Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzi bar
Balozi Seif Ali Iddi alisema Ujenzi wa Taifa imara popote pale hupatikana
kutokana na misingi madhubuti inayoandaliwa katika Sekta ya Elimu na kutekelezwa
ipasavyo chini ya usimamizi wa walimu.
Kauli hiyo ameitoa katika mahafali ya
10 ya Arusha Modern School kwa wanafunzi wa Maandalizi, Msingi na Sekondari
zilizofanyika katika bwalo la Skuli hiyo liliopo Mtaa wa Kisongo nje kidogo ya
Mji wa Arusha.
Balozi Seif alisema msingi huo huwajengea wanafunzi wakati
wamalizapo masomo yao uwezo wa kufanyakazi kwa kujiamini wakati wanapoajiriwa
katika Taasisi tofauti na hata wale wanaoamuwa kujiajiri wenyewe au kuanzisha Miradi
ya Kujitegemea.
“ Lazima mjielewe kwamba nyinyi
wanafunzi ni watu muhimu sana katika hatma ya baadaye ya Taifa. Lakini hii
haitachipuka tuu bila ya kufanya juhudi za kusaka Elimu itakayokidhi mazingira
ya kisasa”. Balozi Seif aliwatanabahisha wanafunzi hao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliwapongeza walimu na wazazi wa Arusha Modern School kwa juhudi zao za pamoja
zilizopeleka wanafunzi wa Skuli hiyo kuendelea kufanya vizuri katika mitihani
yao ya mwaka.
Balozi Seif alisema matokeo hayo mazuri yameijengea sifa nzuri
skuli hiyo na kuwa miongoni mwa skuli bora kimkoa na hata Kitaifa nchini katika
matokeo ya jumla ya kila mwaka.
“Mwaka 2010 darasa la 12 skuli hiyo
ilishika nafasi ya 15 Kimkoa na nafasi ya 234 Nchi nzima ,lakini hatimae
ikapanda na kufikia nafasi ya pili kimkoa na 38 Nchi nzima kwa mwaka 2011”.
Alisisitiza Balozi Seif.
Alieleza kwamba Arusha Medrn School
ni moja ya skuli inayoendelea kutoa mchango mkubwa wa elimu katika Taifa
kutokana na juhudi zake za kuunga mkono Serikali za kutoa Elimu kwa Kundi kubwa
la Vijana ambalo limo katika kujipatia taaluma ndani ya sekta binafsi.
Balozi Seif aliwataka wanafunzi hao
kutobweteka na kiwango cha elimu walichokipata na badala yake waongeze juhudi
zaidi katika masomo yao ya ngazi ya juu.
Alisisitiza kwamba thamani ya
mwanaadamu katika dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia hupimwa kutokana na
kiwango chake bora cha elimu alichokuwa nacho.
Akizungumzia suala la wimbi la dawa
za kulevya linalooonekana kulikumba kundi kubwa la Vijana Balozi seif aliwaasa wanafunzi hao kujiepusha na makundi
ya kihuni yanayoweza kuwashawishi kujiingiza katika vitendo viovu.
Alisema njia bora ya kupita kwa
wanafunzi hao ni kujikita zaidi katika masomo yao pamoja na kufuata ushauri na
mafunzowanayopewa na walimu pamoja na wazazi wao.
Katika risala yao wanafunzi hao wa
elimu yha Maandalizi, Msingi hadi Sekondari wa Arusha Modern School walisema
juhudi za walimu wao zimewawezesha kupelekea kumudu vyema masomo yao hasa
katika mfumo wa sasa wa mabadiliko ya Teknolojia.
Wanafunzi hao walielezea furaha yao
kutokana na wazazi wao kushuhudia kiwango bora cha elimu ambacho wanaimani
kwamba kitawawezesha kuendelea na masomo yao yajayo wakiwa mahiri na kujiamini.
Mapema Mwalimu Mkuu wa Arusha Modern
School Bw. Phillip Wasire alieleza kwamba
mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya skuli hiyo yanatokana na
Heshima kubwa yha wanafunzi wao iliyotanguliwa na ushirikiano wa karibu kati ya
Wazazi, Uongozi wa Skuli pamoja na Wanafunzi wenyewe.
Bw. Phillip Wasire alisema Uongozi wa
Skuli hiyo utahakikisha sifa hiyo ya Heshima iliyojengeka Skulini hapo
itaendelea kupewa umuhimu wa kipekee kwa lengo la kuongeza kiwango bora cha Taaluma.
Katika kutanua wigo wa Taaluma zaidi
Mwalimu Mkuu Wasire alifahamisha kwamba uongozi wa Skuli hiyo imefikiria hatua
ya kuanzisha masomo ya Uhandisi pamoja na mafunzo ya uendeshaji Ndege ili
kuwajengea uwezo wa ajita wanafunzi hao
wakati wanapomaliza masomo yao.
Katika Mahafali hayo yaliyotawaliwa na burdani tofauti
zilizoandaliwa na wanafunzi hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi alikabidhi vyeti kwa wanafunzi waliomaliza masomo yao ya Maandalizi,
Msingi na Sekondari pamoja na kutoa zawadi Maalum kwa wanafunzi wa Darasa la 12
na la 14waliopata Daraja la juu katika
mitihani yao ya Taifa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
0 comments:
Post a Comment