Akinamama Nchini wamekumbushwa kuendelea kuwa wavumilivu ndani ya matukio ya uvunjifu wa amani Nchini yanayoonekana  kujichomoza katika baadhi ya wakati ambayo wakiyashabikia waathirika wakubwa ni wao na watoto.
Kumbusho hilo limetolewa na Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi wakati akiufungua Mkutano  Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania { UWT } Mkoa wa Mjini uliofanyika hapo katika ukumbi wa Mikutano wa Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.
Mama Asha Alisema Dunia imekuwa ikishuhudia madhara yanayowakumba akina mama na Watoto kutokana na mwanzo wa cheche ndogo zinazoachiwa kuchochoewa na baadhi ya watu na vikundi kwa maslahi yao binafsi bila ya kujali athari inayoikumba Jamii yote husika.
Alisema suala la amani limekuwa likisisitizwa na Viongozi kila wakati na kutajwa hata katika Vitabu vya dini lakini baadhi ya watu wamekuwa wakilifanyia mzaha unaopelekea kudharau hata maamrisho hao ya Dini .
Akizungumzia Uchaguzi Mama Asha aliwataka wanachama hao wa UWT kuhakikisha kwamba watu watakaowachagua ni wale watakaokiongezea nguvu za uwajibikaji Chama chao kwa kuwa watetezi safi wa Sera na Ilani ya CCM wakati wote.
Alisema  udhaifu wa baadhi ya Viongozi uioonekana kukipatia mtikisiko chama chao unatokana na ile tabia ya Wanachama kuwapa nafasi watu ambao wanaingia kwenye Uongozi kwa kuzingatia zaidi maslahi yao binafsi.
“ Wapo baadhi ya watu wanaojifanya kuvaa nguo za Kijani na manjano wakati wa mchana na kuhubiri sera za Chama huku usiku wakizibeza sera hizo na kusahau kwamba ndio zilizowapatia fursa hiyo inayowapelekea kuwa na kiburi”. Alifafanua Mama Asha.
“ Ukweli ni kwamba  hata kama ni mpenzi, ndugu au rafiki yako lakini kama hafai huwajibiki kumpa fursa hiyo ya Uongozi kukuongoza”. Atakutia shimoni tu siku moja. Alitanabahisha Mama Asha.
Aliwataka Wanachama hao wa UWT kufanya kazi kwa ushirikiano mara wamalizapo uchaguzi wao kwa lengo la kuiwezesha Jumuiya hiyo kuwa muhimili mkubwa wa Chama cha Mapinduzi.
Akitoa Taarifa fupi ya kazi za UWT Mkoa Mjini Katibu wa Jumuiya hiyo BibiAsia Juma Khamis alisema kumekuwa na maendeleo ya Ustawi wa Jamii kufuatia Wanawake wengi kukubali kujiunga katika vikundi vya ushirika.
Bibi Asia alisema hatua hiyo imezingatia zaidi kuwawezesha Wanawake wengi kujikita katika dhana nzima ya kujitegemea ili kuondokana na utegemezi ambao umekuwa mzigo katika familia nyingi nchini.
Katibu huyo wa UWT Mkoa Mjini alielezea kwamba Jumuiya hiyo imelaani kitendo cha vurugu zilizojitokeza wakati wa Uchaguzi wa Jimbo la Bububu hivi karibuni ambazo zimeleta sura mbaya katika muelekeo wa Demokrasi Nchini.
Alisema Wananchi wengi na hasa wale wanawake wa Chama cha Mapinduzi walikosa kutumia fursa hiyo kwa kuhofia maisha yao kutokana na vitisho vilivyoandaliwa na baadhi ya Vijana wa Kihuni.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Wanachama hao wa UWT Mkoa Mjini  Katibu wa CCM Mkoa Mjini Magharibi Al Hajj Rajab Kudya alimpongeza Mama Asha Suleiman Iddi kwa michango yake mbali mbali anayoitoa ndani ya Chama hicho kupitia Jumuiya zake.
Al Hajj Rajal alimtaja Mama Asha kuwa ni Mwanamke bora katika kuendeleza Chama Cha Mapinduzi ambae mchango wake umeiwezesha CCM kujivunia katika Maendeleo ya  Jumuiya zake.
Katika Ufunguzi huo Mama Asha Suleiman Iddi alichangia Shilingi Laki Nne           { 400,000/- } kusaidia harakati za uchaguzi za Jumuiya hiyo ya Wanawake Tanzania { UWT } Mkoa Mjini.
Othman Khamis Ame 
 Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar                              

0 comments:

 
Top