Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa linalotarajiwa kuanza hivi karibuni hapa Zanzibar.
Amesema suala la vitambulisho limekuwa na umuhimu wa kipekee duniani katika kutunza kumbukumbu na mipango ya kitaifa, hivyo wananchi wasipuuze kujiandikisha kwa ajili ya vitambulisho hivyo.
“Hivi sasa tunasikia kuna baadhi ya maeneo wananchi waliokataa kuhesabiwa katika sense ya watu na makaazi iliyomalizika hivi karibuni nchini kote, hawapatiwi huduma katika maeneo yao, kwa hivyo nakunasihini sana wananchi musipuuze kabisa”, alisisitiza.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanachama wa CUF na wananchi baada ya kufungua tawi la Chama hicho katika jimbo la Magogoni Wilaya ya Magharibi Unguja.
Aidha Maalim Seif aliwaonya watendaji wanaoendelea kuwahangaisha wananchi wakati wanapoomba kupatiwa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi kuwa, kuwa wanakwenda kinyume na maagizo ya Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohd Shein, na kwamba watachukuliwa na hatua za kisheria kwa kukaidi amri hiyo.
Amesema katika baadhi ya maeneo yakiwemo mikoa ya Pemba pamoja na Mkoa wa Kaskazini Unguja, hali ya upatikanaji wa vitambulisho hivyo imekuwa ikienda vizuri lakini tatizo kubwa zaidi limekuwa likijitokeza katika Mkoa wa Mjini Magharibi, jambo ambalo halitofumbiwa macho.
Akizungumzia kuhusu nia ya kujiuzulu kwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Mhe. Ismail Jussa Ladhu, Maalim Seif amewathibitishia wanachama juu ya ukweli wa jambo hilo, na kuwataka wasifadhaike kwani anafanya hivyo kwa nia njema.
“Jussa bado ni mwanachama kindakindaki wa CUF na ni mjumbe wa baraza kuu la uongozi ndani ya Chama chetu, lakini baada ya kutuletea maoni yake nikiwa mimi, Profesa Lipumba na Makamu Mwenyekiti Mhe. Machano Khamis, tuliona sababu zake ni za msingi na hakuna haja ya kumzuia kutimiza maamuzi yake”, alisema.
Ametaja sababu za msingi zilizotolewa na Jussa kutaka kujiuzulu kuwa ni pamoja na kumuwezesha kupata muda wa kutosha kushugulikia maendeleo ya jimbo lake la Mji Mkongwe pamoja na kufanya utafiti kabla ya kuibana serikali katika vikao vya Baraza la Wawakilishi.
Katika Mkutano huo, Maalim Seif alikabidhi baiskeli tisa kwa ajili ya makatibu wa matawi ya CUF katika Jimbo la Magogoni, kigari kwa ajili ya bwana Ali Khamis Ali (mwenye ulemavu), pamoja na shilingi laki tatu kwa ajili ya kikundi cha ushirika cha Jimbo hilo.
Hassan Hamad (OMKR).

0 comments:

 
Top