Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema Jumuiya za Chama Hicho zinaweza kukosa  ufanisi kutokana na tabia ya baadhi ya  Viongozi kudharau Wanachama waliokubali kujitolea kuimarisha Chama hicho.
Kauli hiyo aliitoa wakati akiufunguwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM  {UVCCM } wa Mikoa Miwili ya Magharibi na Mjini hapo katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya CCM Mkoa Uliopo Amani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema  ipo tabia chafu iliyojengeka ndani ya chama ya baadhi ya Wanachama kumuepuka mwanachama anayepoteza muda na nguvu zake kwa ajili ya kutetea na kukisimamia chama katika utekelezaji wa Sera zake.
Aliwataka Wanachama na Viongozi hao wa Umoja wa Vijana wa CCM {UVCCM} Kuhakikisha  kwamba wanawachagua Wanachama wanaoelewa wajibu na dhamana zao  katika Jumuiya na Chama chenyewe.
Alifahamisha kwamba Umoja huo wa Vijana pamoja na ule ya Wanawake              { UWT } ndio mkono mkubwa na mrefu ndani ya chama cha Mapinduzi kwa sababu ya nguvu na wingi wao. Hivyo upo wajibu kwao kuhakikisha wingi na nguvu hizo zinalindwa na kuenziwa ipasavyo.
Aliwatahadharisha Vijana hao kuwa makini katika ulinzi wa Chama chao kwa vile zipo dalili zilizoanza kujichomoza za kuvamiwa kwa Jumuiya hiyo kwa malengo ya watu wachache wanaoelekeza nguvu zao katika uchaguzi wa urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wa Mwaka 2015.
“ Kinacholeta tabu hivi sasa ambacho Vijana wameanza kutumiwa ni nafasi ya Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Mwaka 2015.Msikubali Jumuiya yenu ikatumiwa kwa maslahi binafsi”. Alitahadharisha Balozi Seif.
Balozi Seif Aliwataka wanachama wote wenye nia ya kutaka kugombea nafasi hiyo ni vyema wakasubiri wakati utakapowadia na liliopo sasa ni kuendelea kushirikiana na viongozi wenye dhamana hiyo katika kuwaletea maaendeleo Wananchi.
Akigusia suala la Muungano Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif aliwakumbusha Vijana hao kwamba CCM Bado inaendelea kutetea sera za Serikali Mbili ambazo kila mpenda Maendeleo ameshahudia ufanisi uliopatikana.
Alisema wapo baadhi ya watu wanaochukia mfumo huo lakini  alisisitiza kwamba wataendelea kuchukia kwa sababu mfumo huo bado unaonekana kupendwa na Wananchi pamoja na  wanachama ambao ndio waamuzi wakati wa  mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Muungano wa Tanzania.
Akimkaribisha Balozi Seif Ali Iddi Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM wa uliokuwa Mkoa Mjini Magharibi anayemaliza muda wake mh. Tauhida Galos Nyimbo aliwaasa Vijana kuelewa kwamba kazi ya Vijana ni ya kujitolea wakati wote.
Mh. Tauhida alisema kwamba tabia ya baadhi ya Wanachama kujaziwa fomu za Uongozi inadhoofisha nguvu za Chama kwa vile muda mwingi wa watu hao hutegemea kupata kipato zaidi badala ya kujitolea.
“ Tunaelewa waliojaziwa fomu wana hulka ya kuuliza posho la kikao kiasi gani, ajira lini pamoja na mshiko upo?”. Alifafanua Mh. Tauhida.
 Mapema akisoma Taarifa fupi Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM wa uliokuwa Mkoa  Mjini Magharibi Magharibi Ndugu Mohd Ali Khalfan alisema suala la uchumi bado linaoneka kuwa na matatizo ndani ya Jumuiya hiyo.
Hata hivyo Ndugu Mohd alisema kwamba Uongozi wa Jumuiya hiyo imejipanga vyema katika kukabiliana na tatizo hilo kwa lengo la  kujitegemea wenyewe bila ya kusubiri mwega wa Chama chenyewe.
Akizungumzia amani Ndugu Mohd alifahamisha kwamba wapo watu baadhi ya watu na vikundi vinavyoendeleza tabia ya kupotosha Wananchi hasa katika  amani na utulivu wa Nchi. Hivyo Jumuiya yao imeahidi kupambana na vitendo hivyo kwa kutangaza sera sahihi za chama cha Mapinduzi.
Katika Mkutano huo Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alikabidhi zawadi za safe za chama kwa Vikundi vya Utamaduni vya Imarisha, Kibati pamoja na Big Star vilivyotolewa na Mwenyekiti huyo wa UVCCM wa uliokuwa Mkoa Mjini Magharibi  kama ishara ya kumbu kumbu na upendo kwa wana CCM hao.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar                              

0 comments:

 
Top