Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF Taifa Profesa Ibrahim Haruna Lipumba amesema Tanzania inahitaji kuwa na viongozi wenye dira watakaoweza kuzitumia rasilimali za nchi kwa maslahi ya WaTanzania.
Profesa Lipumba ametoa changamoto hiyo katika viwanja vya Levolosi jijini Arusha, alipokuwa akizungumza na wanachama na wapenzi wa chama hicho, ikiwa ni sehemu ya operesheni mchakamchaka hadi 2015 iliyoandaliwa na chama hicho katika mikoa mbali mbali nchini.
Amesema Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi zikiwemo jiografia yake, bahari na madini  ambazo bado hazijatumika vizuri kuwanufaisha Watanzania wanaoendelea kuishi katika hali ngumu ya kiuchumi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad amewakebehi wale wanaobeza maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa Zanzibar, na kwamba maridhiano hayo yalikuwa ni maamuzi ya Wazanzibari wenyewe na haifai kuyabeza.
Amesema maridhiano hayo yaliyopelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa yameifanya Zanzibar kuwa mfano wa kuigwa kwa Tanzania na nchi nyengine za Afrika Mashariki.
Mapema akisoma risala ya wanachama wa CUF Wilaya ya Arusha, Katibu wa Chama hicho katika wilaya hiyo bwana Hassan Zakaria Zani, amesema wananchi wa Arusha wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbali mbali zikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana pamoja na siasa za vurugu.
Katika mkutano huo Prof. Lipumba alimkabidha kadi ya CUF aliyekuwa Diwani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kata ya ERERAI Mkoani Arusha Bw. John Bayo, baada ya kuamua kukihama chama hicho, sambamba na kukabidhi kadi kwa wanachama wapya walioamua kujiunga na CUF.
 Hassan Hamad (OMKR). 

0 comments:

 
Top