Wanachama wa Chama cha Mapinduzi
Nchini wakati wote wanapaswa kuzingatia
umadhubuti wa Wanachama wanaowachagua katika kushika nafasi za Uongozi wa Chama
hicho kwa nia ya kuhakikisha wanazitetea na kuzilinda Sera pamoja na Ilani ya
Chama hicho.
Kauli hiyo imetolewa na Mjumbe wa
KAmati Kuu ya Halmashauri Kuuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Idi wakati
akiufungua Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa CCM Wilaya ya Kaskazini B
uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Strand iliyoko Kiwengwa
Wilaya ya Kaskazini B.
Balozi Seif alisema tabia ya baadhi
ya wanachana wa CCM kuchagua Viongozi kwa kuzingatia misingi ya Ujamaa, Ukabila
au kujuana inafaa kuepukwa haraka kwa
vile imeshaonyesha ufa ndani ya chama hicho.
Alisema Jahazi la Chama cha Mpainduzi
kuelekea katika harakati za kuimarisha
nguvu za chama hicho hasa kwenye uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015 lazima
liongozwe na manahodha madhubuti watakaokuwa na uwezo wa kuhimili mikikimikiki.
“ Tunataka Viongozi watakaokuwa
tayari kutetea kwa nguvu zote sera na
Ilani za chama cha Mapinduzi bila ya kutafuna maneno”. Alisisitiza Balozi Seif.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa pia Mbunge wa Jimbo la Kitope aliwaomba
Wanachama na Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kukataa kuburuzwa na watu au
vikundi vinavyoeneza uchochezi hasa suala muhimu la Maoni ya Katiba Mpya.
Alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini
Unguja kwa kwa uamuzi wake wa kupiga marufuku mikutano yote inayoashiria cheche
ya kuvunjika kwa amani ndani ya Mkoa huo.
Alisema suala la Katiba ipi inafaa
kuliongoza Taifa la Tanzania limo ndani ya Maamuzi ya Wananchi wenyewe bila ya
kushirikisha maoni au matakwa ya watu, mashirika au Mataifa ya Nje.
Alikumbusha kwamba Sera za Chama cha
Mapinduzi zinaendelea kusisitiza Mfumo wa Muungano wa Serikali mbili ambazo
faida zake zinaonekana na kila mpenda maendeleo ndani ya Ardhi hii.
Balozi Seif alifahamisha kwamba
Muungano uliopo wa Sera za Serikali mbili imeshuhudiwa kupanua harakati za
Kiuchumi, Biashara na hata masuala ya Kijamii pamoja na matumizi muhimu ya
Ardhi kwa Jamii ya Upande Mmoja wa Muungano huo.
“ Anayesema Muungano uliopo haufai inafaa Msemaji huyo
ajiangalie kwanza na inaonekana wazi kwamba yeye ndie asiyefaa”. Alifafanua
Balozi Seif Ali Iddi.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya Tifa ya CCM aliwapongeza Wana CCM wote waliojitokeza kuomba nafasi tofauti za
Uongozi ndani ya Chama hicho ngazi ya Wilaya.
Balozi Seif alifafanua kwamba majina
ya Wanachama yaliyorejeshwa Wilayani Baada ya uchambuzi wa Vikao vya Juu vya
Chama hicho yamezingatia vigezo vilivyokubalika ndani ya chama chenyewe ambao
ni utaratibu uliowekwa na wanachama wenyewe.
Hata hivyo aliwataka wanachama
waliopungukiwa na sifa za uteuzi huo wasikate tama na badala yake waongeze
bidii ya kuchapa kazi kwa nia ya kujijengea uwezo wa kuongoza Chama hicho hapo
baadaye.
Mapema Katibu wa CCM Mkoa wa
Kaskazini Unguja Bibi Caterine Piter Nao alisema Chama cha Mapinduzi Wilaya ya
Kaskazini B kinatarajia kutoa Tamko rasmi kufuatia Vitendo vinavyoendelea kutolewa na Baadhi ya
Viongozi wa Kisiasa na Kidini dhidi ya
Viongozi wa Juu wa Kitaifa hapa Nchini.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Wajumbe
wenzake wa Mkutano huo wa Uchaguzi wa CCM Wilaya ya Kaskazini B Mzee Ali Ameir
Mohd alisea wapo baadhi ya Viongozi wa Chama hicho wanajaribu kuendeleza tabia
za ubabaishaji kitendo ambacho kinafaa kupigwa vita na Wanachama wote wa Chama
hicho.
Mzee Ali Ameir alitahadharisha kwamba
Kiongozi au Mwanachama yoyote atakayeshindwa kutetea Sera za Chama hicho hafai
na anafaa kuepukwa kabisa kuendeleza uozo wake ndani ya chama hicho.
“ Hakuna kazi ndogo ya kulinda
Mapinduzi ya Zanzibar. Nitafurahi nikifa hali ya kuwa naendelea kutetea na
kulinda sera na ilani ya chama cha Mapinduzi”. Alisisitiza Mzee Ali Ameir Mohd
kwa nguvu zake zote.
Mkutano huo Mkuu wa Uchaguzi wa CCM
Wilaya ya Kaskazini B. Ulikuwa chini ya usimamizi wa Mjumbe wa Kamati ya Siasa
ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkwajuni { CCM
} Mh. Jadi Simai Jadi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment