Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. jakaya
Mrisho Kiwete alisema Bara la Afrika linaweza kufanikiwa kuondokana na Janga la
Umaskini na Njaa endapo Jamii za Mataifa hayo zitajikita zaidi katika kuwa wazi
na kushirikiana pamoja.
Rais Kikwete alieleza hayo wakati
akiufungua Mkutano wa Pili wa Ushirika wa Mageuzi ya Kijani ya Afrika { African
Green Revolution Forum - AGRF } wa siku
tatu unaofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya Ngurdoto Mkoani Arusha ambao pia
umehudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa
niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Sheni.
Alisema hakuta kuwa na njia ya mkato kwa Bara hili
kuelekea kwenye Kilimo imara bila ya kuwa na
mipango makini itakayosimamiwa na Washirika wa sekta hiyo zikiwemo Taasisi za
Umma,Sekta Binafsi na Jumuiya za kiraia
ikitiliwa maanani zaidi Vituo vya Utafiti katika maeneo ya Kilimo hasa
Vijijini.
Rais Kikwete alisisitiza kwamba
Wakulima wengi ndani ya Bara la Afrika katika maeneo ya Vijijini wanakabiliwa
na Taaluma duni inayochangia kudumaza uzalishaji katiika sekta ya Kilimo.
Alifahamisha kwamba jembe la mkono
linaloendelea kutumiwa na Wakulima walio wengi Barani Afrika linapunguza nguvu za Wakulima
hao katika uzalishaji na hatimae kuzindisha matatizo na mapungufu katika Sekta
hiyo muhimu.
“ Nguvu nyingi za Wakulima wadogo
wadogo Barani Afrika zinaishia katika jembe la Mkono ambalo hutumiwa na
wakulima waliowengi hasa Vijijini”. Alisisitiza Rais Kikwete.
Alieleza kuwa Kilimo kinaendelea kuwa
chanzo kikubwa cha utajiri wa Afrika licha ya kuwa sera ambazo hazikuhitaji na
kutiliwa maanani katika miongo kadhaa
iliyopita.
Hata hivyo alifafanua kwamba Kilimo
kitaendelea kuwa msingi wa usalama wa chakula na maendeleo ya Kiuchumi.
Aidha alieleza kuwa dhamira iliyopo
ya pamoja iliyojumuisha makundi mbali mbali ya sekta ya Umma na zile Binafsi
katika Mkutano huo wa Pili wa Ushirika
wa Mageuzi ya Kijani Barani Afrika
inaweza kushawishi muelekeo wa mageuzi na uwekezaji kwenye Kilimo cha
Bara la Afrika.
Alisema Kilimo kinaajiri zaidi ya
asilimia 65% ya nguvu kazi Barani Afrika na kinaendelea kuongoza uchumi wa
Mataifa mengi ya Bara hili ikiwa ni kati ya asilimia 60% na 80% ya mapato ya
ndani.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania aliupongeza Uongozi wa Ushirika wa Mageuzi ya Kijani ya Afrika { AGRF
} kwa uamuzi wake wa kuufanya Mkutano huo wa Pili Nchini Tanzania uamuzi ambao
umeipa heshima kubwa Tanzania katika Nyanja za Kimataifa.
Kupitia Mkutano huo Rais Kikwete pia
alimpongeza Mwenyekiti mwenza ambaye pia ni muanzilishi wa Mfuko wa Kimataifa
wa Misaada Bibi Melinda Gates kwa juhudi zake za kuendelea kuunga mkono
harakati za Kiuchumi na Kijamii za Mataifa maskini Duniani ikiwemo Tanzania.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa salamu katika Mkutano huo kwa niaba ya
Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Sheni alisema mkazo unaendelea kuchukuliwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwajengea uwezo Wakulima Wadogo
wadogo.
Balozi Seif alisema Mkazo huo umewekwa kupitia msaada wa Shirika
la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo { IFAD } sambamba na uimarishwaji wa Kituo
cha Utafiti wa Kilimo kiliopo Kizimbani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
alieleza kuwa Zanzibar bado imekipa Kilimo
kipaumbele katika kumkomboa Mwananchi
ambapo zaidi ya asilimia 80% ya watu wote wanategemea Kilimo ambacho ni sekta
muhimili kwa Uchumi na Maendeleo ya
Taifa.
Mapema Mwenyekiti wa Ushirika wa Mageuzi ya Kijani
ya Afrika ambaye pia ni Katibu Mkuu Mstaafu wa Umojwa Mataifa Dr. Koffi Annan
alisema Afrika inahitaji kuongeza nguvu katika kuwajengea uwezo wa uzalishaji
Wakulima wadogo wadogo hasa kutokana na asilimia 60% ya Ardhi ya Bara hili kuwa
ni jangwa.
Dr. Annan alisema ni vyema Wataalamu wakaangalia zaidi mbinu
bora za kuimarisha miundo mbinu katika maeneo ya Vijijini ili kupambana na
changamoto zilizopo kwa kutumia mbinu za kisasa za Kilimo.
“ Mafanikio ya Bara la Afrika katika
kutanuka Kiuchumi kutategemea miundo mbinu ya uwekezaji katika maeneo ya
wakulima wadogo wadogo hasa Vijijini”. Alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Ushirika
wa Mageuzi ya Kijani ya Afrika { AGRF } Dr. Annan.
Aliongeza kwamba mbinu hizo ni vyema
zikaenda sambamba na ushirikishwaji wa
Sekta Binafsi pamoja na uendelezwaji wa Sekta ya utunzaji wa Mazingira.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza ambae
pia ni muanzilishi wa wa Mfuko wa Kimataifa wa Misaada Bibi Melinda Gates
ameipongeza Tanzania kwa hatua yake ya kuimarisha Sekta ya Kilimo kupitia
Mpango wake wa Kilimo kwanza.
Aliahidi kwamba Taasisi yake
itaendelea kuunga mkono jitihada za Mataifa kadhaa ulimwenguni katika harakati
zao za kujikwamua na umaskini na kuondokana na maradhi.
Mkutano huo wa Pili wa Ushirika wa
Mageuzi ya Kijani ya Afrika { AGRF } umehudhuriwa na Washiriki zaidi ya elfu
moja kutoka Taasisi, Jumuiya na Mashirika mbali mbali ya ndani na nje ya Bara
la Afrika.
Othman
Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment