Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya vurugu  vilivyotokea wakati wa uchaguzi mdogo wa Uwakilishi jimbo la Bububu wiki iliyopita ambavyo vilipelekea watu kadhaa kujeruhiwa.
Amesema vitendo hivyo vimeiletea sifa mbaya serikali ya umoja wa kitaifa ambayo iliundwa kwa ajili ya kuendeleza amani ya nchi iliyotoweka kwa kipindi kirefu.
Akizungumza na baadhi ya wahanga wa tukio hilo huko makao makuu ya chama hicho Mtendeni Zanzibar, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema haikutarajiwa kuwa vitendo hivyo vingetokea wakati huu ambao serikali inatekeleza maridhiano ya kisiasa yaliyopelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Amesema pande zote mbili zina wajibu wa kuheshimu na kuyalinda maridhiano hayo katika jitihada za kuendeleza umoja wa Wazanzibari, na kuvishutumu vyombo vya ulinzi kwa kuingilia na kuharibu uchaguzi huo.
Amesema ni jambo la kusikitisha kuona kuwa vyombo vilivyohusika na vurugu hizo havijachukuliwa hatua yoyote, na kwamba bado chama chake kinasubiri kuona hatua zitakazochukuliwa dhidi ya vyombo vya ulinzi vilivyohusika na vurugu hizo.
Akizungumza kwa niaba ya wahanga wa tukio hilo, Mbunge wa Jimbo la Mtoni Unguja kutoka chama hicho Mhe. Faki Haji Makame ambaye alikamatwa kwa tuhuma za kupigana hadharani, amevitupia lawama vyombo vya ulinzi kwa kukubali kutumiwa na wanasiasa kwa maslahi ya vyama vyao.
Kwa mujibu wa taarifa za chama hicho, watu wapatao 22 wakiwemo wanawake, walijeruhiwa katika vurugu hizo za Bububu zilizotokea tarehe 16 mwezi huu kufuatia harakati za uchaguzi mdogo wa Jimbo hilo.
Hassan Hamad, OMKR

0 comments:

 
Top