Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif
Hamad amesema mabalozi pamoja na idara ya mambo ya nje Zanzibar, wanayo nafasi
kubwa ya kuisaidia Serikali kukuza mahusiano yake na nchi nyengine pamoja na
mashirika ya kimataifa.
Amesema licha ya suala
la mambo ya nje kuwa la Muungano, lakini yapo baadhi ya mambo ambayo Zanzibar
inaweza kuyafanya katika kushirikiana na mataifa mengine, kwa lengo la kukuza
uchumi wan chi.
Maalim Seif ametoa
changamoto hiyo ofisini kwake Migombani Zanzibar, alipokuwa na mazungumzo na
Mkurugenzi wa mambo ya nje ofisi ya Zanzibar, balozi Silima Kombo Haji.
Amefahamisha kuwa Zanzibar
kama nchi imekuwa ikitembelewa na viongozi mbali mbali wa nchi za kigeni pamoja na mashirika ya kimataifa
ambao wamekuwa na hamu na shauku ya kutaka kuendeleza mahusiano na Zanzibar,
katika nyanja tofauti zikiwemo za kiuchumi.
“Wakuu wa nchi mbali
mbali wanakuja hapa Zanzibar pamoja na viongozi wa mashirika ya kimataifa, na
huwa na shauku kubwa na kutaka kuendelea mahusiano baina yao na nchi yetu”,
alieleza.
Amempongeza mkurugenzi
huyo kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo, na kwamba serikali itampa mashirikiano
ya kutosha katika kutekeleza majukumu yake, na kusifu kazi nzuri inayofanywa na
ofisi hiyo.
Hata hivyo Makamu wa
Kwanza wa Rais amemtaka mkurugenzi huyo na ofisi yake kwa ujumla, kuongeza
umakini wakati wanaposhughulikia safari za viongozi wakuu wa nchi, ili
kuondosha usumbufu unaoweza kujitokeza.
Kwa upande wake balozi
Silima ambaye alikwenda kujitambulisha kufuatia uteuzi wake wa hivi karibuni,
amemuhakikishia Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa ofisi yake itafanya kazi kwa
karibu na serikali katika kuhakikisha kuwa Zanzibar inapata fursa
zinazostahiki.
Wakati huo huo Makamu
wa Kwanza wa Rais amekutana na uongozi wa Jumuiya ya tiba asilia Zanzibar
JUTIJAZA, na kubadilishana mawazo juu ya maendeleo ya tiba hiyo nchini.
Katibu Mkuu wa Jumuiya
hiyo Dkt. Haji Juma Msanifu amesema jumuiya yake ina mpango wa kuanzisha vitalu
maalum vya miti asilia, ili kurahisisha upatikanaji wa dawa hizo.
Dkt. Msanifu amesema
wamefikia uamuzi huo kufuatia kuendelea kwa vitendo vya ukataji wa miti ovyo,
hali inayotishia kutoweka kwa miti inayotumika kwa ajili ya upatikanaji wa dawa
asilia.
Nae Naibu Katibu Mkuu
wa Jumuiya hiyo bi Zahra Hassan amesema jumuiya yao bado inakabiliwa na tatizo
la ofisi za uhakika pamoja na usafiri, na kuiomba serikali kuangalia namna ya
kuisaidia ili kuondokana na matatizo hayo.
Amesema tiba asilia ni
muhimu na zimekuwa zikitumika kitaalamu na kujipatia umaarufu mkubwa katika
nchi za Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla, jambo ambalo linapaswa kupewa
msukumo kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Maalim Seif kwa upande
wake amewataka wanajumuiya hao kufuatilia upatikanaji wa hati miliki za viwanja
walivyonavyo kwa ajili ujenzi wa ofisi na kituo cha utafiti, ili waweze
kufanikisha matarajio yao kwa uhakika.
Kuhusu ukataji wa miti,
Maalim Seif amesema bado ni changamoto inayoikabili ofisi yake, lakini
wanaendelea kuifanyia kazi ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu ya
kutosha juu ya uhifadhi wa miti na mazingira kwa ujumla.
Hassan Hamad, OMKR.
0 comments:
Post a Comment