Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeushauri Uongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya TransWorld yenye Makao Makuu yake Nchini Dubai kuangalia maeneo ambayo inaweza kuweka Vitega Uchumi vyake hapa Zanzibar.
Ushauri huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati alipokutana na Ujumbe wa Kampuni hiyo hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif aliueleza Ujumbe huo unaoongozwa na Mwenyekiti wa Makampuni ya Transworld ambaye ni mzaliwa wa Zanzibar Bwana Abdallah Karusi kwamba uwekezaji wa Makampuni hayo hapa Zanzibar unaweza kusaidia maendeleo na Ustawi wa Jamii wa Wananchi pamoja na ongezeko la mapato kwa Makampuni hayo.
Alisema kwa vile Kampuni hiyo inajihushisha na Miradi tofauti ya Kimataifa ni vyema kwa Watalaamu wake kuja hapa Zanzibar kukutana na Viongozi wa Taasisi husika na baadaye kuangalia na kuona miradi wanayoweza kuwekeza kwa faida ya pande zote mbili.
Mapema Meneja Mkuu wa Masoko wa Kampuni ya Transworld Mhandisi Adil Abdull Jalil alisema Kampuni yao imekuwa ikijihusisha na miradi ya Miundo mbinu ya Habari na Mawasiliano { IT }, Usafiri wa Anga, Umeme, Mafuta pamoja na Sekta ya Utalii.
Mhandisi Adil Abdul Jalil alisema Kampuni yao imekuwa na Mashirikiano ya karibu na Makampuni mbali mbali ya Kimatifa katika Mataifa ya Marekani, Ufaransa, Dubai sambamba na na eneo la mashariki ya Kati.
Mhandisi Adil aliutaja mradi wa Usafiri wa anga pekee umefikiwa uwekezaji wa gharama ya zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni Mia Saba { 700,000,000 U$ } miradi inayoendeshwa kwa takriban miaka 35 sasa tokea kuasisiwa kwa Kampuni hiyo ya Kimataifa.
Naye Mwenyekiti wa Makampuni ya Transworld Bwana Abdallah Karusi  aliisifu Zanzibar na Kubarikiwa kuwa na mazingira mazuri katika miradi ya Uwekezaji Vitega Uchumi.
Bwana Abdalla alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba uwezo wa kuifanya  Sekta ya Mawasiliano kuwa ya Kimataifa zaidi inawezekana iwapo Uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utashirikiana na Makampuni yanayonia ya kutaka kuwekeza Nchini.
Mkutano huo pia ulishirikisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Othman Masoud Othman, Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Nchi Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Nd. Khamis Mussa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi maendeleo ya Makazi, Maji na Nishati Nd. Mwalimu Ali Mwalimu na Mkurugenzi wa Taasisi ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } Ndugu Salum Khamis.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  aliangalia harakati za ukatwaji wa muembe katika eneo la Magomeni ambao ulikuwa ukilalamikiwa na Wakaazi wa eneo hilo kwamba ulikuwa katika mazingira  hatarishi kutokana na waya wa umeme uliokuwa chini ya matawi yake.
Katika ziara hiyo Balozi Seif aliwaka Viongozi wa Taasisi zinazohusika na maamuzi kuchukuwa hatua mara moja mara tuu linapotokezea tatatizo badala ya kusubiri malalamiko kutoka kwa Wananchi.
Hata hivyo Balozi Seif aliwatahadharisha Wananchi kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya pembezoni mwa Bara bara kwa ajili ya ujenzi wa vibanda vya Biashara ambavyo baadaye huleta usumbufu wakati wa upanuzi wa bara bara.
 Othman Khamis Ame                                                        
 Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top