Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amerejea nchini leo baada ya kumaliza ziara yake ya wiki mbili nchini Marekani na Uingereza.
Maalim Seif aliondoka nchini tarehe mosi mwezi huu kwa ajili ya kuhudhururia mkutano wa kimataifa unaohusiana na masuala ya demokrasia duniani, ulioandaliwa na taasisi ya National Democratic Institute katika mji wa North Carolina nchini Marekani.
Baada ya kumaliza mkutano na makongamano yaliyoandaliwa na taasisi hiyo, Makamu wa Kwanza wa Rais aliendelea na ziara yake katika miji ya Washington na London ambako alikutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa nchi hizo, pamoja na viongozi wa   wa taasisi zinazoshughulikia sera za mahusiano ya kimataifa.
Akiwa mjini Washington, Maalim Seif alikutana na msaidizi Waziri wa mambo ya nje wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika Bwana John Carlson katika jengo la Wizara hiyo mjini Washington, kuzungumzia juu hali ya maendeleo ya siasa na demokrasia Zanzibar.
Pia alikutana na uongozi wa shirika la misaada la Marekani USAID, pamoja na kuzungumza na viongozi wa jumuiya ya wazanzibari wanaoishi nchini Marekani.
Huko Uingereza Maalim Seif alikutana na mabalozi wa nchi za Afrika pamoja na maveterani wa Uingereza, ambao walikutana kuzungumzia masuala mbali mbali yanayohusu maendeleo ya Zanzibar tangu kuundwa kwa serikali ya Umoja wa kitaifa.
Hassan Hamad (OMKR)

0 comments:

 
Top