Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko
tayari kuwasaidia Vijana waliotengemaa baada ya kuacha matumizi ya dawa za
kulevya kwa kuwapatia mtaji endapo vijana hao wataamaua kubuni na hatimae
kuanzisha miradi ya kujiimarisha Kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Viongozi na
baadhi ya Vijana waliomo ndani ya nyumba saba za kurekebishia tabia Unguja kwa
watu waliokuwa wakitumia dawa za kulevya hapo katika moja ya nyumba
hizo iliyopo Mtaa wa Nyarugusu Shehia ya Pangawe Wilaya ya Magharibi.
Balozi Seif alisema Serikali kupitia
Wizara inayosimamia masuala ya Ajira ina mpango wa kuwawezesha Wananchi hasa
Vijana kujiendesha kimaisha katika dhana
nzima ya kuwajengea mazingira ya kuchapa kazi kwa vile Vijana ndio nguvu kazi
kubwa inayotegemewa na Taifa.
Alisema kazi kubwa inaendelea
kufanywa kupitia Taasisi, Jumuiya Washirika wa Maendeleo kwa kushirikiana na Serikali ya kubadilisha tabia kwa Watu na hasa Vijana
kuacha kuendelea kutumia dawa za kulevya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
alizinasihi Familia zenye Vijana wanaotumia au kuathirika na matumizi ya dawa
hizo kuacha hulka ya kuwatenga Vijana wao jambo ambalo linaweza kuwazidishia
kutumbukia katika janga hilo kwa kukosa ushauri pamoja na msaada.
Balozi Seif alisema katika
kukabiliana na tatizo hilo ni vyema kwa Familia hizo kujenga tabia ya
kufuatilia kwa kina Vijana wao walioko katika Nyumba za Kurekebisha Tabia kwa
lengo la kuwarejesha katika mazingira yao ya kawaida.
Aliwapongeza Vijana hao walioamua
kuacha matumizi ya dawa za kulevya kwa hiari yao na kuwataka wahakikishe
wanajilinda kwa nguvu zao zote kuwepuka kurejea katika matumizi hayo hatari kwa
afya zao.
Alisema vitendo hivyo walivyokuwa
wakivifanya kabla vimewasababishia kupungukiwa na akili, Maarifa na hata nguvu
kazi zao zilizokuwa zikitegemewa na familia pamoja na Taifa kwa ujumla.
“ Tusipokuwa na hadhari Taifa
linaweza kuangamia kwa kukosa nguvu kazi ya Vijana hasa kwa kuzingatia kuwa
takwimu zilizopo zinaeleza kuwa wengi wa Vijana waliotumia dawa za kulevya
wameathirika na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi. Sasa hii ni balaa”.
Alitahadharisha Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alishauri
ipo haja kwa Jamii kwa kushirikiana na Serikali Kuu pamoja na washirika wa
Maendeleo kutafuta mbinu za kuwajengea mazingira bora Vijana walioacha matumizi
ya dawa hizo ili wajiepushe kurejea katika magenge ya kihuni.
Mapema Mlezi Mkuu wa Nyumba saba za
kurekebishia Watu wanaotumia dawa za kulevya Zanzibar Bibi Fatma Sukwa alisema
asilimia 42% ya watu waliopitia katika
Nyumba hizo wameacha matumizi ya Dawa za kulevya katika kipindi cha miaka
mitatu.
Bibi Fatma alifafanua kwamba asilimia
48% ya Vijana waliopitia Nyumba hizo wamerejea kutumia dawa za kulevya baada ya
kutengwa na Familia zao, asilimia 1% hadi sasa hawajuilikani taarifa zao tokea
waondoke katika Nyumba hizo.
Mshauri huyo Mkuu wa Nyumba za
kurekebishia tabia kwa watu waliotumia dawa za kulevya ameitahadharisha Jamii
kuelewa kwamba dawa za kulevya ni ugonjwa kama magonjwa mengine
yanayowazunguuka wanaadamu.
Kwa upande wake Mshauri wa kuacha
dawa za kulevya na kubadilisha tabia katika nyumba saba za kurekebishia tabia
za Unguja na Pemba Bwana Ahmed Islam alisema Jamii inapaswa kuacha tabia ya
kuwanyooshea vidole Vijana walioathirika kutokana na matumizi ya dawa za
kulevya.
Bwana Ahmed Islamu alimpongeza na
kumshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa msaada wake ambao
ni faraja kwao ukionyesha kuyathamini makundi hayo ya Vijana .
Katika ziara na Mkutano huo Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar alikabidhi msaada wa Baskeli kwa Kijana Mlemavu Sabri
Ameir Issa ili iweze kumrahisishia harakati zake za kimaisha.
Shughuli hiyo pia ilikwenda sambamba
na Viongozi na Vijana hao wa nyumba za kurekebishia tabia kukabidhiwa msaada wa
vyakula kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.
Balozi Seif alikabidhi Msaada huo kwa
Mshauri Mkuu wa Nyumba hizo za kurekebishia watu walioathirika na matumizi ya
dawa za kulevya Bibi Fatma Sukwa.
Othman
Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment