Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amewataka waumini wa dini ya kiislamu kuungana ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoikabili dini hiyo.
Amesema waislamu wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mbali mbali kutokana na kukosa umoja na mshikamano, jambo ambalo linapaswa kupigwa vita katika kukabiliana na changamoto hizo.
Akizungumza na waumini wa dini ya kiislamu katika msikiti mkuu wa Ijumaa mjini Arusha, Maalim Seif amesema waislamu wamekuwa wakikubaliana katika mambo mengi ya msingi, lakini hutofautiana na kugombana kwa mambo madogo ambayo hayaleti faida kwao.
Asema wakati umefika kwa waislamu kuungana na kuwa na sauti moja katika kupigania maendeleo ya dini hiyo, sambamba na kuandaa miradi itakayosaidia maendeleo ya dini ya kiislam.
Makamu wa Kwanza wa Rais amewahimiza waislamu wenye uwemo kuchangia maendeleo ya dini yao, badala ya kushabikia na kutoa fedha nyingi kuchangia mambo yanayokwenda kinyume na maadili ya dini hiyo.
Maalim Seif ametumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa dini hiyo kuwaelisha wafuasi wao juu ya utoaji wa maoni kwa ajili ya mchakato wa marekebisho ya katiba ya Tanzania unaoendelea katika mikoa mbali mbali nchini.
Amesema hiyo ni fursa pekee kwa waislamu kuweza kutoa maoni yatakayosaidia kuwepo kwa katiba itakayojali maslahi na fursa kwa waislamu kikatiba, ikiwa ni pamoja na kupatiwa nafasi za uongozi katika ngazi mbali mbali serikalini.
Mapema akizungumza katika msikiti huo Sheikh Hashim Lema aliwatanabahisha waislamu kuacha kuogopa kuitangaza dini yao, na badala yake waelimishane juu ya umuhimu wa kuitangaza dini hiyo kwa uwazi, sambamba na kulaani vitendo vinavyolenga kuidhalilisha dini hiyo.
Waislamu kadhaa walipata fursa ya kumuuliza Makamu wa Kwanza wa Rais masuala mbali mbali  yakiwemo mustakbali wa Baraza la Mitihani la Taifa kufuatia malalamiko ya waislamu juu ya kuwepo hujuma kwa matokeo ya mitihani dhidi ya watahiniwe wenye majina ya kiislam.
Akijibu swali hilo Maalim Seif amesema serikali imekuwa ikipata shinikizo kutoka kwa wananchi juu ya haja ya kuanzishwa Baraza la mitihani la Zanzibar, lakini kwanza imeamua Mawaziri wa Elimu kutoka Bara na Visiwani wakutane ili kufanya mazungumzo juu ya namna ya kutatua kadhia hiyo.
 Hassan Hamad (OMKR)

0 comments:

 
Top