Utekelezaji wa kazi za Chama Cha Mapinduzi { CCM }
utakuwa rahisi iwapo Viongozi wapya wa Umoja wa Vijana wa CCM watajipanga vyema
katika kutekeleza majukumu yao watayopewa kwa mujibu wa katiba na Sera za Chama
hicho.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Kaskazini
“B” Mama Asha Suleiman Iddi alieleza
hayo wakati akiufungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Umoja wa Vijana wa CCM
Wilaya hiyo uliofanyika katika Ofisi ya
CCM Jimbo la Kitope uliopo Kinduni Wilayani humo.
Mama Asha alisema bila ya Vijana hao kujituma ipasavyo
Chama chao hakitakuwa na uwezo wa kupiga hatua za haraka za Maendeleo ambayo
ndio nguvu itakayokiwezesha kujijengea uzoefu wa ushindi katika chaguzi zote
zijazo.
Aliwataka Vijana hao kusimama kidete katika kuwakataa Watu wanaogombea uongozi
wakiwa na sura mbili hata kama watu hao watatumia uwezo wao wa kifedha.
“ Wakati wa kuyakataa mapandikizi ndani ya chaguzi
zetu kipindi hichi umefika. Lazima tuyapembue mapumba yanayotukorofisha na tuwe
makini katika kuchagua Viongozi wenye uchungu na Nchi”. Alitahadharisha Mama
Asha Suleiman Iddi.
Mama Asha aliwaomba Wanachama hao wa Umoja wa Vijana
wa CCM kutowarejesha madarakani Viongozi wa chama hicho ambao tayari
wameshaonyesha nia ya kuzipinda sera za Chama chao.
Alifahamisha kwamba Wapo baadhi ya Viongozi, Watu na
hata Vikundi vya Kidini vinavyotaka Nchi hii isitawalike kwa kueneza kasumba ya
kupinga kila linalotakiwa na kupangwa na
Serikali.
“ Tayari tumeshakuwa na Amani, Utulivu na maelewano
ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inayofuata mfumo wa Umoja wa Kitaifa. Sasa inakuaje tena kunajitokeza kasumba
zisizoeleweka mwanzo wala mwisho wake?”. Aliuliza Mama Asha.
Mjumbe huyo wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kaskazini
“B” aliupongeza Uongozi uliopita wa Umoja huo wa Vijana wa CCM ambao
umekiwezesha Chama cha Mapinduzi na Jumuiya zake ndani ya Wilaya hiyo kufikia
hatua makini ya utekelezaji wa sera zake.
Mapema Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Wilaya ya
Kaskazini “B” Ndugu Ali Khamis Ali alisema uchaguzi wa Umoja huo ngazi za
Matawi na Majimbo umekwenda vyema kama
ulivyokadiriwa.
Ndugu Ali alisema umefika wakati kwa Wanachama wa
Umoja huo kuwachaguwa Viongozi wazuri zaidi ya wote ambao waliomba nafasi za
kuuongoza Umoja huo.
“ Ni furaha ilioje kwa Vijana hao ambao ndio majeshi
ya Chama cha Mapinduzi kumaliza chaguzi hizo kwa ufanisi wa hali ya juu”.
Alifafanua Katibu wa UVCCM wa Wilaya hiyo.
Kwa upande wake akitoa shukrani zake baada ya ufunguzi
wa Mkutano huo wa Uchaguzi wa UVCCM Kamanda wa Vijana wa Wilaya ya Kaskazini B
Ndugu Khamis Salum Ali alieleza kwamba Uomja huo utahakikisha unaisaidia
Serikali Kuu katika utekelezaji wa Sera za Chama cha Mapinduzi zilizopata
ridhaa ya Wananchi na kupelekea kuingia madarakani.
Nd. Khamis alisema moja ya Sera zilizomo ndani ya
chama hicho ni kusimamia suala la amani na utulivu ambayo inaonekana kuanza
kuchezewa na baadhi ya Watu na hata vikundi vya Dini.
“ Ukweli hatutakuwa tayari kuona amani yetu iliyomo
ndani ya Wilaya na Mkoa wetu wa
Kaskazini wanakuja watu kutaka kuichezea. Kwa hili tutaonekana wabaya”.
Alitahadharisha Kamanda huyo wa UVCCM Wilaya ya Kaskazini “B”.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment