Balozi mpya wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tavaku Manongi amesema Uongozi wake utajitahidi kuangalia maeneo yanayoigusa Zanzibar moja kwa moja katika jitihada za kunyanyua Uchumi na kustawisha Maendeleo ya Jamii.
Balozi Tavaku akiambatana na Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa Balozi Ramadhan Mwinyi Muombwa alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Nyumbani kwake Mtaa wa Namanga Mjini Dar es salaam.   
Alisema yapo masuala  ambayo Zanzibar ina fursa ya kuyafanya na kuyafuatilia bila ya kuathiri yale maeneo ambayo hushughulikiwa moja kwa moja kwa mujibu wa taratibu za Kimuungano. 
Balozi Tavaku alisisitiza kwamba utendaji wake mara zote utazingatia  zaidi Umoja na Ushirikiano kati yake, Watendaji atakaowaoongoza pamoja na Taasisi, Jumuiya na Nchi washirika.   
“ Nitahakikisha muda wangu pia nautumia katika kuangalia maeneo yanayoigusa Zanzibar kuyafanyiam kazi katika muda wangu wote” Alisisitiza Balozi Tavaku.  
 Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza nguvu na msimamo wa Tanzania katika ushiriki wake kwenye Nyanja za  Kimataifa.  
Balozi huyo wa Tanzania Umoja wa Mataifa alimuomba Balozi Seif kuendelea kuwapa msaada watumishi hao wapya kutokana na uzoefu alionao wa muda mrefu kwenye masuala ya Kimataifa.   
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimpongeza Balozi Tavaku kwa kuteuiwa kushika wadhifa huo na kumtaka awe makini katika kupambana na changa moto zitakazomkabili katika utumishi wake huo mpya.
Balozi Seif alimueleza Balozi Tavaku kwamba miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja mchakato wa Tanzania kuelekea katika katiba mpya ambayo tayari Wananchi wameanza kutoa maoni yao. 
Alisema yapo matatizo katika katiba ya sasa na kitachozingatiwa zaidi katika fursa ya Wananchi ya  utoaji wa maoni ni kuhakikisha kasoro na upungufu uliopo unaondoshwa kwa kujenga katiba madhubuti itakayokidhi mahitaji ya Jamii yote ya Watanza.  
“ Naamini Katiba mpya ijayo kwa kuwa itahusisha Wananchi wote itaondowa kero na mapungufu yaliyokuwa yakileta migongano miongoni mwa Wananchi wa pande zote”. Alifafanua Balozi Seif.
Othman Khamis Ame   
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top