Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alisema Mmiliki wa Kiwanja
kilichopo maeneo ya pembezoni mwa Bwawa la
Mwanakwerekwe Bwana Mwalimu Mussa Khamis
anaweza kuendelea na ujenzi wa nyumba katika Kiwanja chake endapo atakubali
kufuata masharti yote aliyoagizwa na Idara ya Mipango Miji.
Balozi Seif alitoa agizo hilo mara baada ya kufanya
ziara ya ghafla katika eneo hilo lililokuwa likileta mgongano kati ya mmiliki
huyo na Taasisi zinazosimamia Mipango Miji, Mazingira pamoja na Baraza la Manispaa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema suala la kuzingatia Mipango
Miji ni la msingi katika kuepuka maafa yanayoweza kuzuilika pamoja na kulinda
mazingira.
Alisema mmiliki huyo alikuwa na uwezo wa kujenga
nyumba yake ya kuishi kwa mujibu wa alivyopatiwa kiwanja hicho na Taasisi zilizohusika
na ardhi lakini kilichojitokeza kwa mmiliki huyo kuchelewa mno kuendelea na ujenzi huo.
“ ulikuwa na uwezo wa kujenga nyumba kwa mujibu wa
mpango wa mwanzo lakini tatizo linalojichomoza ni kuchelewa mno ambapo yapo
mabadiliko makubwa ya kimazingira katika eneo hili kwa hivi sasa”. Alisisitiza
Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
alimshauri mmiliki wa kiwanja hicho kwamba kama
tayari ameridhia masharti ya mamlaka ya mipango miji ataruhusiwa kuendelea na
ujenzi wake.
Akitoa ufafanuzi wa tatizo hilo Kaimu Mkurugenzi wa Mipango Miji Bwana
Abdulla Salum Rashid alisema taasisi yake ilizuia ujenzi huo baada ya mmiliki
huyo kuamua kutaka kujenga jengo la Biashara la Ghorofa mbili.
Bwana Abdulla alisema pendekezo la mwanzo lililotolewa
na Taasisi zinazosimamia masuala ya ardhi lilimtaka mmiliki wa kiwanja hicho kujenga
jengo la makaazi.
“ Kwa mujibu wa Mipango Miji ushauri uliotolewa jengo
la eneo hilo liwe la Makaazi kama
pendekezo la mwanzo lilivyoelekeza na sio jengo la Biashara tena la ghorofa
mbili”. Alisisitiza Bwana Abdulla.
Mapema Mmiliki wa Kiwanja hicho Bwana Mwalimu Mussa Khamis
alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif kwamba alipatiwa kiwanja hicho kwa mujibu wa taratibu za ugawaji wa
Viwanja kutoka Taasisi za ardhi tokea mwaka 1999.
Bwana Mwalimu alisema amekuwa akipata vikwazo vya
ujenzi huo na kupelekea Mhandisi wake kushindwa kuendelea na ujenzi kutokana na
kukosa kibali cha ujenzi wakati taratibu zote tayari zilikuwa zimeshakamilika.
Eneo hilo
la Kiwanja cha Bwana Mwalimu Mussa Khamis kiliopo kandoni mwa Bara bara iendayo
Fuoni nyuma ya Bwana la Mwanakwerekwe kimepata athari ya kimazingira kutokana
na kuchimbwa ovyo kwa mchanga katika miaka ya nyuma.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment