Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema serikali inathamini mchango mkubwa unaotolewa na waganga wa tiba asilia, na kwamba itaendelea kushirikiana nao katika kutunza afya za wananchi.
Amesema kutokana na mafanikio yanayopatikana kutokana na tiba asilia, serikali inatoa umuhimu wa kipekee kwa tiba hiyo, pamoja na kuandaa mazingira yatakayoziwezesha shughuli za tiba hizo ziende vizuri kwa maslahi ya jamii na taifa kwa jumla.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo katika maadhimisho ya miaka kumi ya tiba asilia barani Afrika, yaliyofanyika katika viwanja vya bustani ya Viktoria mjini Zanzibar .
Amesisitiza haja kwa Wizara ya Afya kuwaungaunisha waganga wa tiba asilia na wale wa hospitali ili kufanikisha malengo ya kuwapatia matibabu bora wananchi wanaosumbuliwa na maradhi mbali mbali.
Amesema kwa sasa waganga hao wamejijengea sifa nzuri ya kitabibu kwa Zanzibar , Afrika Mashariki, bara la Afrika na duniani kote, kutokana na maendeleo yao ya kutumia vipimo vinavyokubalika kabla ya kutoa tiba.
Ametoa wito kwa waganga wa tiba asilia kuacha tabia ya kuficha ujuzi walionao, na badala yake wautumie na kuurithisha kwa wengine ili uwe endelevu kwa maslahi ya vizazi vijavyo.
Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais amewataka wananchi kuutumia muda uliobakia kujitokeza kuhesabiwa katika zoezi la sensa ya watu na makaazi linaloendelea nchini kote.
Amesema suala la sensa halihusiani na itikadi yoyote bali ni kwa manufaa ya nchi na wananchi wake.
Mapema akizungumza katika hafla hiyo,  Naibu Waziri wa Afya Dkt. Sira Ubwa Mamboya  amesema Wizara yake inakubaliana na tiba asilia na inatumika kama dawa mbadala kwa maradhi mbali mbali.
Akizungumzia kuhusu mafanikio ya tiba asili kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita,  Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili Zanzibar Bi. Mayasa Ali amesema ni pamoja na kusajili waganga wa tiba asili mia moja na sabini na moja (171) Zanzibar, kuanzishwa kwa sheria ya tiba asili, kukuza ushirikiano wa waganda wa tiba asili barani Afrika na kupatiwa mafunzo katika nchi za China na India. 
Amewataka waganga wa tiba asili pamoja na wale wa dawa za kisunna kushirikiana na Baraza lake katika kuhakikisha kuwa wanasajiliwa ili kufanya shughuli zao kwa uhakika.
 Hassan Hamad (OMKR).

0 comments:

 
Top