Taasisi inayoshughulikia Taaluma ya Teknolojia ya Afya
ya chuo Kikuu cha Brown Mjini Boston Nchini
Marekani { Med International } imelenga kuisaidia Zanzibar katika Sekta ya Afya ili kufikia
kiwango kinachokubalika Kiteknolojia.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mwenza wa Taasisi
hiyo Bwana Han Shen Chia wakati
akikabidhi Ripoti ya utafiti wa Afya uliofanywa na Wataalamu wa Taasisi hiyo
katika Hospitali za Unguja na Pemba.
Bwana Han Shen akiwa pamoja na Mwakilishi na
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ya Med International
Bwana Jayson Marwaha alisema utafiti huo uliochukuwa takriban wiki 10 umejaribu
kutoa hali halisi ya mapungufu na maeneo ambayo Taasisi yao inaweza kusaidia kitaaluma na hata uwezeshaji.
“ Faraja ilioje na la kutia moyo kuona baadhi ya
vitengo vya uchunguzi wa matumbo { utra sound } na sehemu za kuhifadhia watoto
wachanga wanaozaliwa kabla ya kufikia muda wake vinatoa huduma kwa asilimia 100%”.
Alisema Mkurugenzi huyo mwenza wa Med Inaternational Bwana Han.
Alisema Mipango inaendelea kuimarishwa ili kuona
Taasisi hiyo inawatumia Wataalamu wa Sekta hiyo kuja kutoa mafunzo kwa Walimu
wa Afya hapa Zanzibar.
Bwana Han alifahamisha kwamba utaratibu wa kuwapata
wataalamu hao hasa wakati wa kipindi cha joto ambacho wanakuwa mapumziko
utazingatiwa zaidi.
Kwa upande wake Mwakilishi na Mkurugenzi wa Med
International Bwana Jayson Marwaha alimueleza Balozi Seif kwamba utafiti wao
kwa kuanzia utaangalia zaidi kuimarisha Hospitali za Mnazi Mmoja Unguja na ya
Chake Chake Pemba.
Bwana Marwaha alisema mpango huo utafuatiwa pia na
Taasisi za Nchi hiyo kuweka vitega uchumi vyao vya Sekta ya Afya hapo baadaye
katika Visiwa vya Zanzibar.
Alifahamisha kwamba uwekezaji huo utazingatia na
kutegemea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itakavyoridhia mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hiyo.
Akitoa shukrani zake kwa hatua za Uongozi wa Taasisi
hiyo ya Med Inaternational katika kusaidia sekta ya Afya Zanzibar Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi alisema juhudi za Taasisi hiyo zimeanza kuonyesha mwanga
wa matumaini katika sekta hiyo muhimu kwa Jamii.
Balozi Seif aliuambia Ujumbe huo wa Med Inaternational
kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
bado ina azma ya kuzijengea uwezo Hospiotali zake za rufaa ili zitoe huduma
katika kiwango kinachokubalika kitaalamu zaidi.
Alisema hospitali Kuu za hapa Zanzibar
bado zinahitaji nguvu zaidi kufikia lengo hilo.
Hivyo ushiriki wa Taasisi hizo washirika wa maendeleo unaweza kwa kiasi kikubwa
kuongeza kasi ya uimarishaji huo.
“ Nimeanza kupata matumaini makubwa ya ujio wenu hapa Zanzibar kufuatia ziara yangu ya mwezi oktoba
mwaka jana nchini Marekani. Hata wenzetu wa Chuo Kikuu cha Florida Nchini humo tunaendelea kuwasiliana
nao ambao nao mwaka jana tulitiliana saini mkataba wa ushirikiano na chuo chetu
Kikuu cha Taifa Zanzibar { SUZA }”. Alifafanua Balozi Seif.
Wataalamu wa Taasisi hiyo inayoshughulikia Taaluma ya
Teknolojia ya Afya ya Chuo Kikuu cha Brown Mjini Boston Nchini Marekani kwa
kushirikiana na Watendaji wa Wizara ya Afya Zanzibar wamemaliza utafiti wao
kabla ya muda waliojipangia wa Tarehe 2/9/2012.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment