Uongozi wa Jumuiya ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar umeshauriwa kuchukuwa juhudi za makusudi za kuandika Historia ya Mji Mkongwe  na mabo yake yanayopatikana kwa lugha ya Kiswahili ili Wananchi wapate fursa zaidi ya uelewa wa Mji wao.
Ushauri huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika hafla maalum ya maadhimisho ya miaka 10 tokea kuasisiwa kwa Jumuiya ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar { JUHIMKO } iliyofanyika hapo katika Jumba la Ajabu liliopo Forodhani Mjini Zanzibar. 
 Balozi Seif alisema uandikwaji wa Vitabu hivyo kwa Lugha iliyozoeleka na Jamii na baadaye kusambaswa sehemu mbali mbali Nchini  itasaidia kumilikisha Historia ya MJI Mkongwe kwa Wananchi walio wengi.   
Alisema Mji mkongwe ni miongoni mwa Miji iliyopata fursa ya kuandikwa sana na wasomi na watafiti wa ndani na nje ya nchi lakini bahati mbaya kwamba lugha inayotumiwa ni Kiingereza ambayo haijuilikana na wanchi walio wengi.  
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Historia hiyo muhimu iliyomo ndani ya Mji Mkongwe ni muhimu kwa Uchumi wa Nchi hii lakini si Wananchi wengi wa Zanzibar wanayoifahamu hasa Vijana.  
“ Ni Vijana wangapi leo wanafahamu Historia ya Ngome Kongwe, Jengo la Beit Al Ajaib pamoja na kujengwa kwa Mahamam ya Hamamni?”. Aliuliza Balozi Seif. 
 “ Mji Mkongwe wa Zanzibar ni Mji wa Historia tajiri inayojuilikana na wageni lakini isiyojuilikana na wenyeji”. Alisisitiza Balozi Seif. 
 Alieleza kwamba changamoto inayowakabili Wazanzibari ni kuhakikisha kuwa ile hadhi ya Mji huu ambayo imepelekea  kujingizwa kwenye urithi wa Kimataifa inabakia pale pale kwa faida ya wananchi na vizazi vijavyo.  
 Balozi Seif alisema kwamba kazi ya kutunza hadhi ya Mji huu inahitaji nguvu kubwa ya mashirikiano kwa pande zote ambazo ni Serikali, Wananchi na hasa jumuiya zisizo za Kiserikali.      
“ Ni vyema tukafahamu kuwa kamahatutoshirikiana kuuenzi Mji Mkongwe wa Zanzibar pamoja na mazingira yake na Utamaduni wa Watu wake , Historian a utambulisho wa Zanzibar Kimatifa utaathirika”. Alitahadharisha Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Jumuiya hiyo ya Hifadhi ya Mji Mkongwe { JUHIMKO } kwa kufuata vyema taratibu za usajili tokea kuanzishwa kwake miaka kumi iliyopita ikiwemo kuwasilisha Taarifa za kazi na ripoti za fedha  kwa mrajisi Mkuu wa Serikali.  
Aliiomba Jumuiya hiyo kuendelea kushirikiana na Wataalamu katika kutoa mwamko kwa wamiliki, wawekezaji pamoja na Wananchi wa Mji Mkongwe  kufuata taratibu za kufanya matengenezo sahihi yasiyofuta Historia ya Mji Mkongwe.                                
Akitoa Historia ya Muundo wa Jmuiya hiyo ya Juhimko Mwenyekiti wa Jamuiya hiyo Bwana Mohammend Juma Mugheiry amesema zipo athari kadhaa za kutoipa umuhimu Taaluma ya uhifadhi hasa kwa upande wa Miji ya Kihistoria katika Nchi zinazoendelea na kufikia hadi kuyakosa maeneo muhimu. 
 Bwana Mugheiry alishauri kwa kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki suala hili linapaswa kupewa uzito unaofaa kwa kuanzisha  mashirikiano yanayohusu uhifadhi wa maeneo ya Kihistoria.  
 Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Hifadhi  Mji Mkongwe amesema Taasisi yao imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa kubwa  ikiwa ni njia za mapato ya kuendeleza  juhudi zilizoanzishwa.
Alisema Jumuiya yao imezoea kupata msaada wa fedha kwa wafadhili wa Nje ambao wanaposita miradi yao hukwama wakati wafadhili wa ndani wanaosaidia baadhi ya mambo hususia kusaidia masuala yanayohusu urithi wa Utamaduni na hasa ufadhili wa majengo ya Kihistoria.      
Bwana Mugheiry aliitaja change moto nyengine ya kutokuwepo kwa Sera ya mambo ya urithi ambayo ameiomba Serikali Kuu kulifanyia kazi suala hili muhimu kwa maslahi ya Taifa.  
Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Juhimko ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Taasisi zake zote zilizopelekea kuipa nguvu jumuiya yao katika kutekeleza malengo yaliyopelekea kuanzishwa kwake. 
 Akitoa shukrani Katibu wa Jumuiya hiyo Ndugu Al-Halil Mirza amempongeza Makamuj wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa kauli yake ya kufikiria kuitaka Wizara ya Elimu Zabzibar kuandaa utaratibu wa Mitaala yake kuliingiza somo la uhifadhi wa Mji Mkongwe wa Zanzibar. 
 Nd. Mirza alisema kufanya hivyo ndio njia pekee ya kuiandaa Jamii kupitia ngazi za Chini kupata Taaluma sahihi ya Historia ya Mji mkongwe  ambao umeteuliwa kuwemo katika urithi wa Kimataifa. 
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mbunge WA Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi Vifaa pamoja na Vyakula kwa ajili ya Wanafunzi wa Skuli za Sekondari za Jimbo la Kitope walioweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mitihani yao.                                               
Balozi Seif alikabidhi Vifaa  na vyakula hivyo  ikiwa ni pamoja na Mchele, Sukari, Mafuta ya Kupikia na harage kwa skuli za Kiwengwa, Upenja, Kilombero  iliyopewa pia Mipira na Seti za Jezi na Fujoni  hapo ukumbi wa Ofisi ya CCM Jimbo la Kitope uliopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini B. 
 Shughuli hiyo ilikwenda sambamba na kukabidhi saruji paketi 25 na Mchanga kwa kila Tawi la CCM la Kichungwani, Kipandoni, Muembe Majogoo na Mfenesini kwa Gube. Akizungumza katika hafla hiyo fupi Balozi Seif alisema hatua hiyo anayoendelea kuichukuwa tokea mwaka uliopita  ina lengo la kushirikiana na wazee wa wanafunzi hao katika kuwapatia utulivu wa Kimasomo katika muda wao wa ziada. 
 Vifaa na Vyakula hivyo vimegharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni Nne, Laki 8 na Tisini na tisa elfu { 4,890,000/- }.
 Othmana Khamis Ame 

0 comments:

 
Top