Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaangalia mazingira ya kuimarisha pamoja na kuvifufua Viwanda Vidogo
vidogo ili kuongeza soko la ajira sambamba na kupata mbinu za usindikaji wa
mazao mbali mbali yanayozalishwa hapa Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizungumza na Balozi Mpya wa India Nchini Tanzania Bwana Debnath Shaw
aliyefika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi.
Balozi Seif alisema Zanzibar
imekuwa na historia kubwa ya masuala ya Viwanda vidogo vidogo hasa katika miaka
ya thamanini jambo ambalo lilileta faraja kwa bidhaa za Zanzibar katika Soko la Mataifa ya Mwambao wa
Afrika Mashariki.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
alimuomba Balozi huyo wa India
Nchini Tanzania kuyashawishi
Makampuni ya Nchi yake kuitumia fursa hiyo ya uwekezaji katika sekta ya Viwanda
kwa lengo la kusaidia Uchumi wa Zanzibar
sambamba na kuongeza mapato ya Makampuni hayo.
Balozi Seif aliipongeza na kuishukuru Serikali ya
India kwa hatua yake inayochukuwa ya kuunga mkono harakati za Maendeleo za
Zanzibar hasa katika masuala ya Uhandisi, Afya na Elimu.
Alisema idadi ya Wanafunzi wa Zanzibar
wanaopatiwa mafunzo mafupi na marefu Nchini India imeongezeka zaidi na kuleta
ufanisi katika Taasisi za Serikali.
“ Ongezeko la idadi ya Wanafunzi wa Zanzibar
wanaopata Taaluma India
imesaidia kuimarisha uhusiano zaidi wa
Kiuchumi na Ustawi wa Jamii kati yetu na Nchi hiyo”. Alifafanua Balozi Seif.
Alimuhakikisha Balozi huyo mpya wa India Nchini Nchini Tanzania kwamba Uhusiano huo wa
muda mrefu kati ya pande hizo mbili utazidi kudumishwa kwa faida ya jamii ya
Wananchi wa Nchi hizo.
Mapema Balozi Mpya wa India
Nchini Tanzania
Bwana Debnath Shaw alisema katika kuunga
mkono Mataifa ya Bara la Afrika Nchi yake yake tayari imeshaandaa Mpango wa
kuongeza ushirikiano wake na Mataifa
hayo ndani ya kipindi cha Miaka mitano iliyopita.
Balozi Debnath alisema mpango huo umelenga zaidi kuyaongezea
nguvu za kiuchumi Mataifa hayo katika masuala ya Taaluma na uwekezaji kwenye
Sekta ya Afya.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alikutana na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa Zanzibar Balozi Silima K. Haji aliyefika kujitambulisha baada ya
kuteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni.
Katika mazungumzo yao
yaliyofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar
Balozi Seif alisema Idara hiyo ni muhimu kwa vile imeundwa maalum kwa ajili ya itifaki ya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
alimueleza Balozi Khamis kwamba Zanzibar
hivi sasa iko katika muelekeo mpya wa
uendeshaji wa Serikali katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa.
Hivyo aliiomba Taasisi hiyo muhimu kutumia nguvu zake
katika kuhakikisha inaitangaza Zanzibar kimataifa ili ieleweke kutokana na mfumo huo
mpya.
Alisema yapo matumaini makubwa ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar
kuendelea kuwa imara kutokana na uwakilishi wa Viongozi wa pande zote mbili
ambazo zilikaribiana katika matokeo ya kura katika uchaguzi Mkuu uliopita.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment