Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema licha ya jitihada zinazoendelea  kuchukuliwa na Uongozi wa Jimbo hilo lakini bado ipo kazi kubwa ya kufanywa katika kufikia Maendeleo bora ya Wananchi wake.
Balozi Seif alisema hayo mara baada ya kupokea kero na changamoto zinazowakabili Wanachama na Wananchi wa Kijiji cha Pangeni hapo katika Ukumbi wa Tawi la CCM la  Kijiji hicho.
Akizungumza na Uongozi wa Halmashauri ya CCM ya Tawi hilo Balozi Seif akiwa pia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema changa moto zinazowakabili Wananchi hao zinaweza kutanzuka kama suala la ushirikiano kati yao na Viongozi wanaowaongoza litapewa nafasi ya pekee.
Balozi Seif alifahamisha kwamba zipo changamoto nyingi ndani ya Jimbo la  Kitope lakini kutokana na hali halisi iliyopo ipo haja ya kuziangalia  zile muhimu zaidi ili zipatiwe ufumbuzi kulingana na uwezo wa uwezeshaji uliopo.
“ Ingefaa sisi Viongozi tukazingalia na kuzipa msukumo zile changamoto ambazo tunahisi zitatekelezeka kwa mujibu wa umuhimu wake zaidi kulingana na hali halisi ya uwezo wetu”. Alisisitiza Balozi Seif.
Aliueleza Uongozi huo wa Halmashauri ya CCM Tawi la Pangeni kwamba Miradi iliyopewa umuhimu wa mwanzo katika kipindi hichi ndani ya Jimbo hilo ni pamoja na uwekaji wa Kifusi kwa Bara bara iendayo Boma pamoja na huduma ya Umeme hapo Kinduni.
Alisema Miradi hiyo miwili itatekelezwa kupitia Mfuko wa Jimbo. Hata hivyo Balozi Seif aliutaka Uongozi wa Tawi hilo kufanya tathmini ya matengenezo ya mbao za madirisha na dari ya Tawi hilo na kupelekewa  ili apate muda wa kufanya maarifa ya ukamilishaji kwa ajili ya ufunguzi rasmi wa Tawi hilo hapo baadaye.
Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope aliwapongeza Wanachana hao wa CCM kwa kuwachagua tena Viongozi wao  na hali hii inatokana na usimamizi wao mzuri katika utekelezaji wa sera za  CCM.
Balozi Seif pia alielezea faraja yake kutokana na Wananchi wengi wa Kijiji hicho kujitokeza kwa wingi katika zoezi la Uandikishaji wa Sensa ya Watu na Makazi.
Alisema hatua hiyo imesaidia kuliweka katika Historia Jimbo la Kitope pamoja na yeye kupata hadhi zaidi kutokana na nafasi yake ya Uwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi Tanzania.
Akizungumzia suala la  Katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Seif aliwaomba Viongozi hao kuwashajiisha zaidi Wanachama wao pamoja na wananchi katika kushiriki kikamilifu kutoa maoni yao wakati utakapowadia.
Alisema Wananchi katika baadhi ya Wilaya hapa Nchini wameshaanza mchakato wa kutoa maoni yao katika hali ya amani na utulivu lakini hata hivyo zipo dalili za cheche za baadhi ya watu kutaka kuharibu hali hizo kwa visingizio vya Dini.
“ Katika suala la amani na utulivu tumeshapiga hatua kwa vile tayari tumeingia ndani ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa lakini cheche za kutaka kuharibu mfumo huu kwa kisingizio cha kukataa muungano imeanza kujichomoza”. Alifafanua Balozi Seif.
Mapema Katibu wa Uchumi na Fedha wa Tawi hilo la CCM Pangeni Ndugu Riyamy Khamis alisema  Kijiji chao bado kinakabiliwa na changamoto kadhaa zinazorejesha nyuma maendeleo yao ya kila siku ikiwa ni pamoja na ukosefu wa Huduma ya Umeme pamoja ukamilishaji wa jengo la Skuli yao.
Alieleza kwamba hakutakuwa na Muungano utakaowasaidia Wananchi waliowengi Nchini Tanzania kwa kuuvunja huu uliopo hivi sasa.
Wakati huo huo Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif alifika katika Ofisi yake ya Jimbo iliyopo Kitope kusikiliza baadhi ya Matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi wa Jimbo lake.
Akipokea matatizo hayo masuala ya ardhi pamoja na harakati za Kijamii ndizo zilizoonekana kuchukuwa nafasi zaidi ya mazungumzo hayo.
Ofisi za Bunge Nchini Tanzania zimejengwa na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuwapatia Wabunge nafasi muwafaka ya kusikiliza kero na changamoto ya wananchi wanaowaongoza katika Majimbo yao.
 Othamn Khamis Ame
Pfisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top