Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amekutana na mabalozi wa nchi mbali
mbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini Marekani na kubadilishana mawazo juu ya
masuala tofauti yakiwemo ya kiuchumi, afya na teknolojia ya habari.
Katika mazungumzo yake
na balozi wa Malaysia nchini Marekani bwana Othman Hashim, Maalim Seif amesema Zanzibar
inaweza kushirikiana na Malaysia katika maeneo mbali mbali ikiwa ni pamoja na
sekta ya elimu ya juu, biashara,
uwekezaji na kilimo.
Maeneo mengine ambayo
Zanzibar na Malaysia zinaweza kushirikiana ni teknolojia ya habari, benki za
kiislamu na utalii.
Katika mazungumzo hayo
viongozi hao pia wamekubaliana juu ya suala la kufuatilia mazungumzo hayo ambapo
Zanzibar itatuma maofisa wake nchini
Malaysia, ili kuona namna ya kukuza mahusiano yaliyopo baina ya nchi hizo
mbili.
Kabla ya kukutana na
mabalozi hao, Makamu wa Kwanza wa Rais alipata fursa ya kushiriki kwenye
mikutano na makongamano mbali mbali juu ya mambo ya siasa na mahusiano ya
kimataifa yaliyoandaliwa na taasisi ya National Democratic Institute mjini
North Carolina, Marekani.
Makamu wa Kwanza wa Rais pia amefanya
mazungumzo na mkuu wa taasisi
inayojishughulisha na utoaji wa misaada ya vifaa vya hospitali katika nchi
mbali mbali duniani Bwana Abdul Makembe Kimario.
Katika mazungumzo yao
viongozi hao walijadiliana juu ya uwezekano wa Zanzibar kuweza kufaidika na
misaada hiyo ya vifaa vikiwemo vitanda
vya kulazia wagonjwa, vitanda maalum vya kufanyia upasuaji na mashine za
uchunguzi wa maradhi mbali mbali katika hospitali zake za Wilaya na hospitali
kuu ya Mnazimmoja.
Taasisi hiyo imekuwa
ikijishughulisha na utoaji wa misaada ya vifaa vya hospitali kwa zaidi ya nchi
124 duniani zikiwemo China, India na Israel.
Maalim Seif pamoja na
viongozi na mabalozi wa nchi mbali mbali pia walihudhuria katika kongamano
maalum, ambapo walishuhudia viongozi wa
vyama vya Republican na Democratic vya nchini Marekani wakihojiwa na waandishi
wa habari kuhusiana na kampeni za uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba 6
mwaka huu nchini humo, ambapo chama cha Demcratic kinawakilishwa na Rais wa
sasa wa Marekani Rais Barack Obama na chama cha Republican kinawakilishwa na
Bwana Mitt Romney.
Makamu wa Kwanza wa
Rais aliwasili nchini Marekani tarehe 02 mwezi huu kwa ziara ya kikazi. Katika
uwanja wa ndege wa New York alipokelewa na Balozi wa kudumu wa Tanzania katika
Umoja wa Mataifa Balozi Tuvaku Manongi na huko Mjini North Carolina alipokewa
na Balozi wa Tanzania nchini Marekani bibi Mwanaidi Sinare Maajar.
By. Mwandishi
Maalum-Marekani.
Imehaririwa na Hassan Hamad (OMKR), Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment