Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anakusudia kumuandikia Barua Waziri anayesimamia masuala ya Ardhi Zanzibar kumtaka kufuta mara moja hati ya umiliki wa Viwanja vya nyumba ambavyo vimo ndani ya eneo la Chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni.
Balozi Seif alitoa kamuli hiyo wakati akiangalia eneo la Chuo hicho ambalo limevamiwa kwa ujenzi ndani ya  ziara yake katika Taasisi zilizomo ndani ya Sekta ya Afya ikiwa ni mwanzo wa ziara zake kuangalia utendaji wa Wizara za Serikali pamoja na changamoto zinazozikabili Wizara hizo.
Balozi Seif akionyeshwa kukasirishwa kwake na tabia ya baadhi ya watu kukaidi maamuzi ya Serikali pamoja na Maagizo ya Mahkama ya kuhodhi ardhi alisema Taifa halitakuwa na Maendeleo kama Jamii ikijali zaidi Ubinafsi.
Aliagiza kusitishwa mara moja maendeleo ya ujenzi wa nyumba moja   ambayo tayari ina mgogoro ulioko mahakamani pamoja na kuzuiwa kwa ujenzi wowote kwa wale waliomilikishwa viwanja saba ndani ya eneo hilo la chuo.
“ Kamwe hatutaacha maendeleo ya Umma kwa kuachia Mtu au watu binafsi. Kwa Tabia hii hakuna namna ya kufanikisha Maendeleo ya chuo kama hakutakuwa na Ardhi”. Alitahadharisha Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahaisha kwamba Serikali haikusudii kufanya ubabe kwa rai wake lakini kamwe haitasita kuchumchukulia hatua za kisheria Raia atakayeonyesha dharau au jeuri dhidi ya Serikali.
Alieleza kuwa haipendezi kuona Washirika na wafadhili wanaendelea kutoa misaada mbali mbali katika uendelezaji wa majengo na Taasisi za Serikali huku Viongozi wansema kuna maeneo ya ujenzi wa Taasisi hizo.
Aliupongeza Uongozi wa Wizara ya Afya kupitia Chuo hicho kwa juhudi zake za kuendeleza Majengo yatakayokidhi mahitaji ya wanafunzi kwa siku za baadae.
Mapema Msimamizi wa Ujenzi wa Chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni Ndugu Waziri Juma alimueleza Balozi Seif kwamba Eneo hilo lilikuwa   likimilikiwa kihalali na Chuo cha Ufundi cha Mbweni tokea mwaka 1962.
Ndugu Waziri  Alisema Chuo cha Sayansi kikilazimika kisheria kuomba eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa chuo chake ambapo baadaye uongozi wa chuo hicho ukaamua kujenga ukuta baada ya kuanza dalili za uvamizi wa eneo hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitembelea Madarasa ya chuo hicho na kuridhika na hatua ya ufundishaji iliyofikiwa na uongozi wa chuo hicho.
Balozi Seif aliangalia shughuli za kila siku ya Maabara ya Kitengo cha Mapambano dhidi ya Maradhi ya Malaria kiliopo Mwanakwerekwe ambapo Meneja Mkuu wa Kitengo Hicho Bwana Mwinyi Mselemu alisema alieleza mkakati mpya wakuiweka Zanzibar huru na ugonjwa wa Malaria.
Alisema Utaratibu unaandaliwa wa kufuatili kesi za wagonjwa wa malaria katika kila shehia kila baada ya wiki mbili kwa lengo la kufanikisha amakakati huo.
Baadaye Balozi Seif alikagua harakati za uchangiaji damu katika Kutoa cha kuchangia damu kiliopo Sebleni ambapo Meneja Mkuu wa Kituo hicho Dr. Mwanakheir Mahmoud alizitaja baadhi ya changamoto zilizopo ni kupungua kwa kasi ya wachangiaji damu.
Akiangalia ujenzi wa Bohari Kuu ya Wizara ya Afya iliyopo ndani ya iliyokuwa kiwanda cha sigara Maruhubi Balozi Seif alielezea kuridhika kwake na hatua hiyo ambayo italeta faraja kwa Wizara ya Serikali ya ujumla.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimalizia ziara yake kwa kuangalia utendaji katika maabara za Hospitali kuu ya Mnazi mmoja pamoja na Bodi ya chakula , Dawa na Vipodozi.
Watendaji wa Taasisi hizo alisema zipo changamoto ambazo serikali kuu inastahiki kuzifanyia kazi zikiwemo baadhi ya mashine zinazohitaji vipuri ambavyo ni  mzigo kugharamiwa na vitengo vyao.
Kwa Upande wake Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi Bw. Burhan Othman Simai alisema yapo mafanikio makubwa kwa Taasisi yake katika mapambano dhidi ya wafanyabiashara wakorofi wanaoshindwa kufuata taratibu na sheria za Nchi.
 Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top