KUHUSU KUUAWA KWA
MWANDISHI WA HABARI WA CHANNEL TEN NA MWENYEKITI WA KLABU YA WAANDISHI WA
HABARI MKOA WA IRINGA (IPC) DAUDI MWANGOSI
Tasisi ya Vyombo vya Habari
Kusini mwa Nchi za Kusini mwa Afrika (MISA Tan) imepokea kwa masikitiko makubwa
taarifa ya kifo cha mwandishi na kiongozi mahiri wa waandishi hapa nchini.
Aidha tunaungana na waandishi na
wafanyakazi katika tasnia ya habari nchini, Chama cha Klabu za Waandishi nchini
(UTPC) pamoja na familia ya marehemu Mwangosi katika kipindi hiki kigumu
ambacho tasnia yetu ya habari imelazimika kuingia matatani kutokana na matumizi
ya mabavu ya JeShi la Polisi.
Tunalaani kwa nguvu zote matumizi
ya mabavu ya polisi ambayo yamesababisha kifo cha mwandishi wa habari akiwa
chini ya ulinzi wa Polisi.
Huu ni mwendelezo wa matumizi ya
nguvu kupita kiasi yanayofanywa na polisi kwa raia wa nchi hii. Ni lini polisi watasimamia ulinzi wa
raia na mali zao badala ya kugeuka kuwa jeshi la mauaji kila wananchi
wanapokusanyika kwa minajili ya kutimiza ndoto zao?
Kifo cha Mwangosi kimegubikwa na
sintofahamu hasa ukijua kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa bwana Michael
Kamuhanda alikuwa anamtambua kama kiongozi wa waandishi wa habari mkoa na
alikuwepo kwenye tukio wakati Mwangosi akiwa mikononi mwa polisi.
Lakini ikumbukwe kuwa siku zote
hata katika vita waandishi wanafanya kazi bega kwa bega na askari ili kuwajuza
wananchi nini kinachotokea kwenye uwanja wa mapambano. Kwa jeshi la polisi hapa
nchini limedhihirisha kuwa baada visa na mikasa kuwatokea raia wa kawaida sasa
wamewageukia waandishi wa habari na kukatisha maisha yao kikatili.
Ikumbukwe pia kuwa wakati mauaji
haya yanatokea kuna mkutano mkuu wa UTPC unaoanza wiki hii huku wawakilishi wa
vyama vya waandishi wa mbalimbali wa kimataifa wakitegemea kushiriki katika
mkutano huo wa mwaka. Na hii itatoa taswira halisi ya jinsi Jeshi la Polisi
linavyofanya kazi hapa nchini.
Jumuiya ya kimataifa itaweza
kujionea hali halisi jinsi waandishi wa habari hapa nchini wanavyofanya kazi
katika mazingira hatarishi na kwamba sasa Tanzania inawezekana isiwe mahali
salama pa kuishi kama walivyokuwa wakisikia kwenye vyombo vya habari vya kwao.
Mfano halisi ni mhanga Daudi Mwangosi ambaye ataingia katika vitabu vya
kumbukumbu duniani kwa mwaka 2012.
Tunaiomba serikali ichukue
maamuzi makini ya kukaa pamoja na vyama vya siasa ili kutafuta njia muafaka ya
kutuliza mikusanyiko ya wananchi kwa njia za amani na sio kutumia mabavu katika
kuwatawanya.
Ni imani yetu kuwa historia
imeonyesha kuwa nguvu kupita kiasi kwa wananchi inaongeza chuki dhidi ya
serikali yao ya wakati huo na kamwe hainyamazishi dukuduku zilizoko mioyoni mwa
wananchi. Kokote kule duniani matumizi ya polisi yalipovuka mipaka yakaamsha
hasira za wananchi na kuzifanya nchi hizo zisikalike.
Matumizi ya mabavu, nguvu kupita
kiasi kuzima vuguvugu za wananchi kwa kile wanachokiamini pamoja na mauaji na
hasa kwa wanahabari na raia wasio na silaha hayajawahi kufanikiwa kokote kule
duniani.
Tunaamini kuwa serikali yetu ni
sikivu na itachukua hatua stahiki. Pamoja na kwamba uchunguzi huru sio
utamaduni wa serikali yetu lakini katika hili la mwandishi akiwa na kalamu na
kamera yake afie mikononi mwa polisi tunahitaji uchunguzi huru na wa kina.
Tumaini Mwailenge
Mkurugenzi,
MISA Tanzania
0 comments:
Post a Comment