WASHINGTON:Makamu wa Kwanza wa Rais wa  Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amewahakikishia Wazanzibari wanaoishi nchi za nje kuwa Serikali imeanzisha Idara maalum kwa ajili ya kushughulikia masuala ya Diaspora ili kuwa karibu zaidi na Wazanzibari walioko nje ya nchi.
Amesema hatua hiyo imelenga kurahisisha mawasiliano kati ya serikali na wazanzibari hao, ikiwa ni hatua muhimu katika kusogeza mbele maendeleo ya nchi na wazanzibari hao.
Maalim Seif ametoa changamoto hiyo alipokuwa akizungumza na viongozi wa Jumuiya ya wazanzibari wanaoishi nchini Marekani ZADIA, katika ukumbi wa hoteli ya Marriott mjini Washington .
Amewapongeza wazanzibari hao kutokana na hatua yao ya kuanzisha jumuiya hiyo, ambayo itasaidia kuunganisha nguvu zao na kuwa na sauti ya pamoja katika kushughulikia masuala mbali mbali yanayohusu maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Amewataka wana-diaspora hao kuangalia uwezekano wa kusaidia harakati za maendeleo Zanzibar , na kuwaasa kutojisahau wakati wanapokuwa nje ya nchi, ili kujiwekea mazingira bora ya maisha yao ya baadae.
Maalim Seif ameelezea umuhimu wa wazanzibari hao kuendelea kutafuta takwimu za wazanzibari wanaoishi nchini Marekani, ili kurahisisha mipango yao na serikali.
Kwa upande wake mwenyekiti wa jumuiya hiyo Bw. Omar Ali, amemueleza Maalim Seif kuwa wazanzibar wanaoishi nje ya nchi wanahitaji kupatiwa nyenzo na mashirikiano ya karibu kutoka serikalini, ili kurahisisha harakati za maendeleo.
Amesema Jumuiya ya ZADIA ina wataalamu wengi wenye ujuzi wa fani mbali mbali zikiwemo elimu, utafiti na ufundi ambao iwapo watatumiwa vizuri wanaweza kuisaidia Zanzibar katika harakati zake za kujitafutia maendeleo.
Mapema Wana-diaspora hao walimkabidhi Maalim Seif nakala ya hati ya usajili ya jumuiya yao ili ziwekwe katika kumbukumbu za  Idara ya Diaspora Zanzibar.
Mwandishi maalum, USA

0 comments:

 
Top