WASHINGTON: Makamu wa Kwanza wa
Rais amekutana na msaidizi Waziri wa mambo ya nje wa Marekani anayeshughulikia masuala
ya Afrika Bwana John Carlson katika jengo la Wizara hiyo mjini Washington,
kuzungumzia juu hali ya demokrasia na siasa za Zanzibar.
Katika mazungumzo yao Maalim
Seif alimueleza kiongozi huyo juu mwelekeo wa utoaji wa maoni ya katiba mpya ya
Tanzania kwa upande wa Zanzibar, kwamba wananchi wamekuwa wakitoa maoni yao kwa
uhuru licha ya kuwepo kwa changamoto
ndogondogo.
Amesema wananchi wengi
wa Zanzibar wamekuwa na mwamko tofauti, huku wengine wakitetea muundo wa
muungano wa serikali mbili kama ilivyo sasa na wengine wakitetea muungano wa
mkataba ambao utaiwezesha Zanzibar kuwa na mamlaka kamili na kutambuliwa
kimataifa.
Makamu wa Kwanza wa
Rais pia amemueleza kiongozi huyo juu ya mafanikio makubwa yaliyopatikana
Zanzibar tangu kuundwa kwa serikali yenye mfumo wa umoja wa kitaifa.
Kwa
upande wake, kiongozi huyo wa Marekani ameisifu Zanzibar kwa jitihada zake za
kuimarisha demokrasia na kuwaletea maendeleo watu wake na kuahidi kuendelea
kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha demokrasia na kuleta maendeleo kwa
Wazanzibari.
Maalim
Seif yuko mjini Washington DC baada ya
kumaliza ziara yake katika mji wa North Carolina.
Wakati huo huo Shirika
la misaada la Marekani USAID limeahidi kuendeleza misaada yake kwa Zanzibar
katika maeneo tofauti yakiwemo kilimo
cha umwagiliaji pamoja na maktaba za vitabu katika wilaya za Unguja na Pemba.
Naibu kiongozi wa
shirika hilo bibi Linda Atim, ametoa ahadi hiyo alipokuwa na mazungumzo na
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika ofisi za
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani mjini Washington.
Bibi Linda mwenye
jukumu la kushughulikia masuala ya Sudan ya kusini na kaskazini pamoja na
Afrika Mashariki, amesema shirika hilo limeridhishwa na matumizi mazuri ya
misaada yake inayoitoa kwa Zanzibar, na kuahidi kuyafanyia kazi maombi
yaliyotolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais kwa shirika hilo.
Katika mazungumzo yake
na uongozi wa shirika hilo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif
Sharif Hamad amelishukuru shirika la USAID la Marekani kwa misaada yake kwa
Zanzibar, na kuliomba kuongeza misaada yake katika maeneo mengine likiwemo kuisaidia
Zanzibar kuweza kujitosheleza kwa chakula kupitia mradi wake wa Feed the
Future.
Pia ameliomba shirika
hilo kufikiria namna ya kuisaidia Zanzibar katika kilimo cha umwagiliaji kwa ekari elfu
sita ambazo hazijaanza kutumika kwa kilimo hicho
Maeneo mengine
waliyojadiliana ni pamoja na uwezekano wa kuisaidia Zanzibar katika kuongeza
uwezo wa wake wa kuhifadhi chakula, pamoja na
kutanua wigo wa teknologia ya habari katika skuli za Zanzibar.
Marekani imekuwa
ikisaidia miradi mbali mbali ya maendeleo kwa Zanzibar ikiwemo mradi wa
kutokomeza malaria ambao upata mafanikio makubwa, mradi wa vitabu maskulini,
miradi ya ujenzi wa barabara pamoja na mradi
wa njia ya Umeme kutoka Dar es Salaamu hadi Zanzibar.
Pia Makamu wa Kwanza wa
Rais amepata fursa ya kutembelea kitengo
cha kupambana na majanga katika Makao Makuu ya Serikali ya Marekani ambapo
alijionea jinsi serikali ya nchi hiyo ilivyojidhatiti katika kupambana na
majanga pamoja na vitisho vya aina
yoyote kutoka ndani na nje ya nchi.
Maalim Seif amesema miongoni
mwa mambo ambayo Zanzibar inaweza kujifunza ni namna serikali inavyoweza kujipanga kabla ya kutokea kwa
majanga, pamoja na kuwa na njia maalum
za uokozi wakati majanga yanapotokea.
Mwandishi maalum, USA.
0 comments:
Post a Comment