Na, Mwandishi Maalum, London
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar yenye muundo mpya wa serikali ya umoja wa kitaifa inafanya
kazi zake vizuri na inakaribisha wawekezaji kutoka sehemu mbali mbali duniani
kwa lengo la kukuza na kuendeleza uchumi wa nchi.
Amesema viongozi wa serikali hiyo kutoka
vyama vya CCM na CUF wamekuwa wakishirikiana vyema na wananchi katika jitihada
za kuendeleza umoja wa kitaifa ambao ulitokewa kwa kipindi kirefu.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo mjini
London Uingereza, alipokuwa akijibu masuali mbali mbali kutoka kwa mabalozi wa nchi
za Afrika pamoja na maveterani wa Uingereza, waliokutana kuzungumzia masuala
mbali mbali yanayohusu maendeleo ya Zanzibar.
Katika masuala yao ya msingi, mabalozi na
maveterani hao walitaka kujua juu ya mustakbali wa Zanzibar pamoja na maendeleo
ya serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka
2010.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
amesema licha ya changamoto ndogo ndogo zilizopo kutoka kwa baadhi ya viongozi na
watendaji wa ngazi za chini, Serikali ya Umoja wa kitaifa imepata mafanikio
makubwa ikiwa ni pamoja na kurejesha umoja wa Wazanzibari pamoja na kuweka
mazingira bora ya kuvutia wawekezaji.
Kabla ya mkutano huo wa mabalozi, Maalim
Seif amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya nje wa
Uingereza anayeshughulikia masuali ya Jumuiya ya Madola bwana Mark Simmonds, katika ofisi za Wizara
hiyo mjini London.
Katika hatua nyengine Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar amekutana na baadhi ya viongozi wa Umoja wa Wazanzibari
Wanaoishi Uingereza Zanzibar Walfare
Association (ZAWA) na kubadilishana mawazo juu ya mambo mbali mbali yanayoihusu
zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarisha idara ya Diaspora, ili iweze kuwa karibu
zaidi na wazanzibari wanaoishi nchi za nje.
Viongozi wa jumuiya hiyo wametaja mafanikio
mbali mbali yaliyopatikana ikiwa ni
pamoja na kuanzisha asasi za kijamii nchii Uingereza ambazo zitawaunganisha wazanzibari
wanaoishi nchini humo.
Jumuiya hiyo pia imeelezea nia yake ya
kuleta maendeleo Zanzibar kupitia jitihada mbali mbali ikiwa ni pamoja na
kujjipanga katika kusaidia vifaa na
vitendea kazi zikiwemo kompyuta.
Kwa upande wake Maalim Seif
aliwasisitiza Wazanzibari wanaoishi nchini Uingereza na kuwataka kuendeleza
umoja na mshikamano wanapokuwa nje ya nchi, sambamba na kufikiria namna
wanavyoweza kuisaidia nchi yao kimaendeleo.
Maalim Seif aliwasili nchini Uingereza
tarehe 12 Septemba 2012, baada ya kumaliza ziara yake nchini Marekani, ambapo
mara tu baada ya kuwasili alitembelea ofisi za ubalozi wa Tanzania mjini London
kwa lengo la kusalimiana na wafanyakazi wa ubalozi huo
0 comments:
Post a Comment