Kikao cha Nane cha Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi Tanzania kimekutana leo  chini ya Mwenyekiti wake Mweza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Hapo katika Ukumbi wa Zanzibar Beach Resort Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. 
 Wajumbe wa Kikao hicho ambao ni pamoja na Mawaziri ,Makatibu Wakuu na Baadhi ya Maafisa wa Takwimu bara na Zanzibar walipata fursa ya kutathmini mwenendo mzima za zoezi la kuhesabu Watu Nchini Lililomalizika mwishoni mwa Wiki iliyopita. 
Akitoa Tathmini ya zoezi hilo la Sensa kwa Upande wa Tanzania Bara Waziri wa Fedha wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. William Mgimwa alisema kwa sasa kazi ya kuhakiki usahihi na kuhariri taarifa zilizokusanywa na Makarani wa Sensa zinaendelea Nchi nzima kwa kutumia miongozo iliyotolewa na Wizara husika.  
 Dr. Mgimwa alisema wasimamizi katika ngazi ya Taifa, Mikoa na Wilaya walikuwa na kazi ya kuhakikisha madodoso ya maeneo yote ya kuhesabia watu katika wilaya zote yameshakusanywa ili kukamilisha awamu ya pili ya Sensa ya watu na makazi.
 Waziri Mgimwa alifahamisha kwamba juhudi za uhamasishaji wa Sensa Nchini umeonyesha mafanikio kutokana na idadi ya watu waliokataa kuhesabiwa haikuwa kubwa hasa Tanzania Bara. 
 Alisema Uhamasishaji uliokuwa ukifanyika katika maeneo mbali mbali nchini kabla ya zoezi la sensa ulilenga kuhakikisha kuwa watu wanapuuza ushawishi wa kukataa kushiriki sensa ulikuwa unatolewa kupitia mihadhara ya kidini, vipeperushi, fulana na baadhi ya vyombo vya Habari. 
 Dr. Mgimwa alieleza kwamba pamoja na changamoto zilizojitokeza, juhudi zilifanyika kuhakikisha waliolala Nchini Usiku wa kuamkia siku ya Sensa walihesabiwa na kwamba walitoa Taarifa sahihi zitakazoisaidia Serikali katika kutunga Sera, kupanga Mipango ya Maendeleo ya Nchi na kutoa maamuzi sahihi. 
 NayeWaziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Omar Yussuf Mzee akitoa thathmini kwa upande wa Zanzibar alisema juhudi zinaendelea za kuimarisha ubora wa kupata idadi ya Watu na kuhakiki madodoso ili kuwa na Takwimu sahihi kwa maendeleo ya Taifa. 
 Mh. Omar Yussuf alieleza kwamba  ipo haja ya kutafutiwa ufumbuzi mambo yatayoathiri ubora wa takwimu kabla ya kuanza kwa mchakato wa uchambuzi wa Takwimu hizo.      Wakichangia wajumbe wa Kikao hicho  waliwapongeza Makarani, wasimamizi pamoja na watendaji wote waliosimamia kuendesha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi. 
Hata hivyo walishauri Viongozi wa Serikali zote mbili za Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kwamba changamoto pamoja na hitilafu zilizojichomoza kabla na baada ya zoezi hilo zisipuuzwe. 
 “ Baadhi ya wanajamii wetu wamekuwa na Utamaduni wa kutumia hoja zinazosambazwa na baadhi ya Watu kwa maslahi yao kinyume na muelekeo wa Taifa”. Alisisitiza mmoja wa wajumbe hao Mh. Mohammed Aboud. 
 Akitoa nasaha zake Mwenyekiti Mwenza wa Kikao hicho cha Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Balozi Seif Ali Iddi alisema ipo haja kwa Serikali zote mbili kujipanga vyema katika kutafakari kasoro zilizojichomoza ndani ya zoezi la Sensa ya watu mwaka huu. 
 Balozi Seif alisema ipo tabia kwa baadhi ya watu wanaoshawishi jamii zinazowategemea kuendelea na hulka ya kupinga kila kitu kinachotolewa au kuagizwa na Viongozi wa Serikali. 
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Mwakilishi wa Jumuiya Aga Khan Foundation aliyepo hapa Zanzibar Bwana Mohd Baloo. 
 Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar Balozi Seif aliipongeza Jumuiya hiyo yenye Makao yake Makuu Mjini Geneva kwa dhamira yake ya kusaidia Maendeleo ya Zanzibar hasa katika harakati za uimarishaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar. 
 Balozi Seif alisema mchango wa Jumuiya ya Aga Khan ndani ya  Mji Mkongwe wa Zanzibar umepelekea ushawishi wa kuwa na mvuto kwa wageni pamoja na watalii wanaotembelea Zanzibar na hatimae kuongeza mapato ya Taifa pamoja na ajira kwa baadhi ya Vijana kupitia Sekta ya Utalii. 
 Mapema Mwakilishi wa Jumuiya ya Aga Khan Foundation hapa Zanzibar Bwana Mohd Baloo alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif kwamba Taasisi yake imekuwa ikijihusisha mara kwa mara na ustawi wa Jamii katika Mataifa mbali mbali Duniani. 
Bwana Baloo alisema Jumuiya hiyo bado inaendelea na mipango ya kuongeza miradi yake ya Kiuchumi itakayosaidia ustawi wa Kiuchumi katika Mataifa washirika Duniani.

0 comments:

 
Top