Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Kayanza Peter Pinda amewataka wamiliki wa MwanaHalisi waende mahakamani wakiona kuwa kulifungia gazeti lao kwa muda usiojulikana hawakutendewa haki.
Waziri Mkuu alikuwa anajibu swali lililoulizwa la papo kwa papo Bungeni Dodoma lililoulizwa na Mbunge wa Jimbo la Hai ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyetaka kujua ni lini gazeti la kiuchunguzi litafunguliwa maana hakuna ukomo wa kufunguliwa kwake.
Waziri Mkuu amesema kuwa sio gazeti tu litakalofungiwa kama likikiuka sheria zilizopo bali chama, taasisi au shirika na mtu binafsi atachukuliwa hatua kali za kisheria iwapo atakiuka taratibu na sheria zilizowekwa.
Mbowe alienda mbali zaidi kwa kuhoji kuwa Sheria ya Magazeti iliyotumiwa kulifungia imepitwa na wakati kwa kuwa ni kandamizi na kwamba hata Jaji Francis Nyalali alipendekeza kufutwa. Waziri Mkuu amesema kuwa hiyo ni sheria halali iliyotungwa na Bunge na haijafutwa kutoka kwenye vitabu vya sheria na kwamba hadi hapo itakafutwa na bunge itakoma kutumika kwake.
Wakati huo huo, Mbunge wa Tabora Mjini Ismael Aden Rage amemuuliza Waziri Mkuu kuwa kwanini serikali haiwachukulii hatua kali wanaotumia nyaraka za siri za serikali na kuzipitisha kwenye vyombo vya habari. Waziri Mkuu kama kawaida yake akasema serikali iko makini katika hilo ila inalegeza kidogo lakini itakapoanza kuzitumia sheria hizo wale wote wanaohusika watachukiwa kama ndege tai.
Katika maendeleo mengine kuhusu suala hilo la MwanaHalisi, kufuatia kikao kilichoitishwa na MISA Tan kujadili suala la kutafuta haraka njia za kuitaka serikali ilifungulie gazeti hilo na kupendekeza njia za kuchukua za haraka, kamati iliyoundwa ili kupanga mikakati inakutana katika kikao chao cha kwanza leo.
Kikao cha pili cha kamati hiyo maalum kitafanyika siku ya Jumamosi ambapo siku ya Jumatano (22/08/2012) kitafanyika kikao kikubwa kitakachohusisha wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu, waanahabari pamoja jukwaa la wahariri ili kuanza utekelezaji wa haraka wa njia za kuibana serikali kuifungulia MwanaHalisi.
Baadhi ya njia zilizopendekezwa ni kuiomba Jumuia ya Kimataifa na tasisi za Umoja wa Mataifa kuifungia Tanzania misaada, kuwafutia vibali vya kusafiri nje viongozi wa serikali katika nchi zao pamoja na kupanga mikakati mingine ya kususia kuishirikisha au kushiriki katika masuala yote ya serikali kwa viongozi waliohusika katika kulifungia gazeti hilo (black out).

0 comments:

 
Top