Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto imeanza utaratibu wa kuwapatia milo mitatu Wazee wanaopatiwa hifadhi ya makazi katika Nyumba za Serikali Sebleni .
Mkurugenzi Utumishi Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto Nd. Iddi Ramadhan Mapuri alieleza hayo mara baada ya futari ya pamoja kati ya Wazee wa Sebleni na baadhi ya Viongozi wa Serikali ambayo iliandaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Nd. Iddi Ramadhan Mapuri alisema uamuzi huo wa Wizara umekuja kufuatia agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohd Sheni la kuitaka Wizara hiyo kulitekeleza mara moja.
“ Inapendeza kuona utaratibu huu tumeanza nao kipindi hichi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani utakuwa wa kudumu”. Alisisitiza Nd.Mapuri.
Mkurugenzi Utumishi huyo wa Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa juhudi zake za kuwa karibu na Wazee hao.
Ndugu Mapuri alisema ukaribu huo wa Balozi Seif umeonyesha namna gani anavyoonekana kuwajali zaidi Wazee hao muda wote.
Nao Wazee hao kwa upande wao wameelezea faraja yao kutokana na mfumo wa Viongozi wa ngazi za juu wa Serikali kuwa karibu nao hasa katika masuala ya Kijamii.
Mzee Hassan Haji akiwakilisha wazee hao wa Sebleni katika shukrani hizo baada ya futari hiyo alisema kitendo cha Balozi Seif Ali Iddi cha kula nao futari ya pamoja kimeonyesha mapenzi kati yao.
Utaratibu wa kufutari pamoja baina ya Waumini wa Dini ya Kiislamu na Viongozi wao umekuwa wa kawaida na kuzoeleka kwa kipindi kirefu sasa hapa Nchini.
Utaratibu huu umekuja kufuatia waumini wa Dini ya Kiislamu kutekeleza mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni moja miongoni mwa nguzo tano za Kiiislamu ambazo humuwajibika kila muumini kuzitekeleza.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top